UKURASA WA 861; Tunaona Kilichopo, Na Siyo Kisichokuwepo…

By | May 10, 2017

Leo sijaumwa mguu,

Siyo kwamba ni kawaida yangu kuumwa mguu, lakini nimefikiria sijawahi kujiambia hivyo. Zipo siku nyingi ambazo siumwi mguu, lakini sijawahi kuchukua muda na kufikiria namna ambavyo siumwi mguu.

IMG-20170214-WA0007

Lakini inapotokea siku moja nimeumwa mguu, mawazo yangu yote yanahamia kwenye kuumwa mguu. Nitafikiria zaidi kuhusu kuumwa mguu, japo mguu nilikuwa nao muda wote, kipya ni maumivu yaliyoanza.

Mfano huu mdogo na unaoweza kuupima kwenye kila eneo la maisha yako, unaonesha namna gani kipaumbele chetu siyo kwenye vitu ambavyo havipo, bali kwenye vitu vilivyopo, vitu ambavyo tunaviona au kuvisikia kwa sasa.

Unapanda gari na kusafiri salama, unapofika mwisho wa safari hushangai kwamba gari halijapata ajali. Lakini gari lolote linapopata ajali, habari kuu inakuwa kuhusu gari kupata ajali. Kinachojadiliwa ni kile kilichopo na siyo ambacho hakipo.

Sasa kwa nini nakwambia yote haya?

Yapo mengi ya kujifunza na kunufaika na hali hii, ila hapa nitakushirikisha haya mawili muhimu.

Kwanza; kwenye kazi yako na biashara yako, hakikisha unaonekana, hakikisha watu wanatambua uwepo wako. Kwa sababu watu wanazungumzia na kufikiria kile kinachoonekana na siyo kisichoonekana. Hivyo kama hufanyi mambo ya kuwafanya wale wanaokulenga waone uwepo wako, unajipotea wewe mwenyewe. Fanya kazi bora, toa huduma nzuri, wafanye watu waone kile unachofanya namna kinaboresha maisha yako, na hapo watakuwa wanafikiria kuhusu wewe. Hii ndiyo sababu matangazo huwa yanasaidia, unaweza kujiuliza tangazo la kampuni au bidhaa fulani lina maana gani, hasa unapoona alama pekee na hakuna maelezo mengi. Wanacholenga ni wewe ujue uwepo wao, ili unapofanya maamuzi yako, uwakumbuke na huenda ukanunua kwao.

SOMA; Vunja Sheria Hizi Za Hovyo….

Pili; kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha hakuna mambo unayoyasahau kwa sababu hayaonekani kwa sasa. Yaani unaweza kuwa unafanya maamuzi yako kwa yale ambayo unayaona pekee, kumbe yapo usiyoyaona ambayo yanaweza kuleta hatari kubwa kwako iwapo hutayazingatia kwenye kufanya kwako maamuzi. Huenda kutokuonekana kwa baadhi ya mambo au vitu ni kiashiria kwamba mambo hayaendi vizuri. Hivyo mara zote, kabla ya kufanya maamuzi, jiulize kipi muhimu ambacho hukioni kwa sasa, lakini kipo na muhimu. Utaifanya akili yako kufikiri zaidi na hivyo kuweza kufanya maamuzi bora kabisa.

Hakikisha unaonekana, na muhimu zaidi, ona kisichoonekana ili kufanya maamuzi bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.