UKURASA WA 870; Kazi Itakayojimaliza Yenyewe…

By | May 19, 2017

Leo rafiki nataka nikuulize kitu kimoja, kuhusu kazi ambayo kila siku umesema utaifanya, ila unaendelea kuahirisha. Hivi unapokuwa unaahirisha unakuwa unafikiria nini? Kwamba hiyo kazi kwa muujiza fulani itakuja ijimalize yenyewe? Au kwa muujiza kesho utaamka ukiwa vizuri kuliko leo na kuweza kuanza au kuendelea kufanya?

Tabia ya kuahirisha mambo, hasa yale muhimu na ambayo ni magumu, ni tabia inayowazuia watu wengi kufanikiwa. Kwa sababu bila ya kufanya hakuna matokeo na bila ya matokeo hakuna mafanikio.

Lakini bado watu wanaendelea kuahirisha mambo, bado watu wanasema watafanya kesho, bado unajiambia ukiwa vizuri utafanya.

Vitu viwili unapaswa kujua kuhusu kuahirisha mambo.

Moja; hakuna kitu kitakachokuja kujikamilisha chenyewe, hata ukasubiri miaka mingapi. Kitu kitafanyika, pale ambapo utaacha sababu na kukaa chini kufanya. Siyo tofauti na hapo, haijalishi utasubiri muda mrefu kiasi gani.

Pili; hakuna siku utakuwa vizuri zaidi ya ulivyo sasa. Chochote unachohitaji ili kuanza tayari unacho au kipo ndani ya uwezo wako. Ni wewe tu uchukue hatua ya kuanza na dunia itaunguka, kukuletea kila unachohitaji ili kuendelea. Lakini siyo kabla haijakujaribu ili kuona kama kweli una ujasiri wa kuendelea.

SOMA; Kazi Ya Maisha Yako Yote…

Hivyo basi rafiki, kuendelea kusubiri hakuna msaada wowote kwako. Hakutapelekea kitu kujikamilisha chenyewe na wala hakukusaidii wewe kuwa bora zaidi ya ulivyo sasa.

Kwa kifupi, kuendelea kusubiri ni kujipotea muda na kuyachelewesha mafanikio. Rudi kwenye yale muhimu ambayo umekuwa unasema kila siku utafanya, na anza kuyafanya sasa. Namaanisha leo hii, angalia wapi pa kuanzia na anza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.