UKURASA WA 883; Kushindwa Ni Ushindi…

By | June 1, 2017

Hakuna ushindi mkubwa kwenye maisha, kama kushindwa. Najua unaweza kuuliza hilo linawezekanaje, inawezekanaje kushindwa kwako kuwe ushindi, au ni kujidanganya na kujibembeleza? Na mimi nitakujibu kwa sababu zifuatazo;

  1. Unaposhindwa, maana yake umejaribu kitu, umefanya kabisa na siyo kwamba umekaa na kupanga tu. Pamoja na hofu zote, umekaa chini na kufanya kitu. Na huo ni ushindi mkubwa sana, kwa sababu wapo wengi ambao wanapanga watafanya kila siku, lakini hata kuanza hawaanzi.
  2. Pia katika kufanya kwako, na kushindwa, yapo mambo muhimu sana ambayo umejifunza, na usingeweza kujifunza kwa namna nyingine yoyote ile. Kwa mfano kwenye kuanzisha biashara, ukikaa na kujifunza biashara pekee, utaona kila kitu kipo sawa, ni mpaka uingie na kufanya, ndipo unakutana na vitu hukuwahi kuvifikiria. Na hapo unajifunza kwa uhalisia zaidi. Hivyo kushindwa kwako, kumekufanya upate somo muhimu sana la njia bora kabisa za kufanya.
  3. Wakati mwingine utafanya kwa utofauti na ubora zaidi. Ni mjinga pekee anayeweza kurudia kufanya jambo lile lile wakati halimpi matokeo anayoyataka. Mwerevu anajifunza na kuboresha zaidi. Kushindwa ni ushindi kwa sababu wakati mwingine hutafanya kama ulivyofanya awali, badala yake utaboresha zaidi na hivyo kuweza kufanya makubwa zaidi.

Hizi ni sababu chache muhimu kwa nini kushindwa kwako ni ushindi mkubwa.

Kushindwa ni ushindi, na kushinda ni ushindi mkubwa zaidi leo. Unaona ilivyo raha, kwamba kila unachofanya wewe ni ushindi. Kwa sababu ukishinda unapata ulichotaka, lakini pia ukishindwa unakuwa umejifunza na kuwa bora zaidi. Huoni namna ulivyo na bahati?

SOMA; Thamani Iliyopo Ndani Ya Kushindwa…

Usisahau hayo yote mawili yanaokana na kitu kimoja tu; KUFANYA. Siyo kupanga wala kuota kutakuletea ushindi tunaosema hapa, bali kukaa chini na kufanya, kufanya haswaa, ndiko kunakuletea ushindi tunaojifunza hapa.

Nimepata wazo la kitabu hapa, nitaandika kitabu, na kwenda ndani zaidi kwenye hili, ili tuweze kuchukua hatua zaidi. Maana najua wengi tunapenda mafanikio, lakini tunaogopa kushindwa, hivyo tunaacha kabisa kufanya. Lakini vipi kama ukijua iwe utashindwa au kushinda bado utakuwa mshindi? Utasukumwa zaidi kufanya. Na kufanya ndiyo jawabu la kila kitu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.