UKURASA WA 895; Uhakika Wa Asilimia 100…

By | June 13, 2017

Hakuna jambo lolote kwenye maisha yetu ambalo tuna uhakika nalo kwa silimia mia moja, hivyo kwa kila tunachofanya, kuna nafasi ya kupata kile tunachotaka kupata, na nafasi ya kukosa.

Japo unaweza kuwa unataka sana kitu fulani kitokee, na ukafanya kila ambacho unapaswa kufanya, bado matokeo yanaweza kuwa tofauti na usiweze hata kusema sababu ni nini.

Nakukumbusha hili rafiki, kwa sababu wengi tumekuwa tunapanga mambo na kujihakikishia kwa asilimia 100 yatakwenda hivyo. Hatujiandai kwa matokeo mbadala, hivyo yanapotokea yanatuumiza sana na kutufanya tushindwe kupiga hatua.

Chochote unachopanga, hata kama unaona nafasi ya kupata matokeo ni kubwa kiasi gani, usiache kuwa na maandalizi kwa matokeo tofauti na unayotegemea. Ona uwezekano wa matokeo tofauti, na kuwa na maandalizi, ukijua ni hatua zipi muhimu utachukua ili kuhakikisha mambo yako hayakwami.

SOMA; Njia Ya Uhakika Ya Kujiongezea Kujiamini…

Na hili halina uhusiano wowote na kuwa chanya au hasi, maana wengi huelewa vibaya dhana hizo. Ni lazima uwe chanya, ukitegemea matokeo bora, lakini pia unapaswa kuwa chanya kwa kujiandaa iwapo matokeo yatakuja tofauti na ulivyopanga. Kuwa na maandalizi ya matokeo tofauti siyo kufikiri hasi, badala yake ni kuhakikisha hukwami kwa namna yoyote ile.

Hakuna jambo lolote kwenye maisha yetu ambalo tuna uhakika wa asilimia 100, lakini kila jambo linaweza kufanyika. Kwa kuwa na maandalizi bora ya akila aina ya matokeo, na kuendelea kuchukua hatua bila ya kukata tamaa, tunaweza kupiga hatua hata tunapokutana na changamoto na vikwazo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.