UKURASA WA 904; Wakati Unapoona Kama Kila Kitu Hakipo Sawa…

By | June 22, 2017

Katika safari ya mafanikio, kuna wakati unaweza kuoka kama kila kitu hakipo sawa. Kwenye wakati kama huo unaweza kuona kama unakosea kila kitu. Huu ni wakati ambapo changamoto zinakuwa nyingi, na unapozitatua unaibua changamoto nyingine. Mambo uliyotegemea hayatokei na hapo ndipo unaona kuna mahali unakosea sana.

Inawezekana ndiyo kuna sehemu unazokosea, lakini hisia unazokuwa nazo kwa wakati huo zinakuwa zimepitiliza. Kwa sababu unaona kama wewe tu ndiye mwenye hali hiyo. Hasa pale unapoona wengine wakiendelea na maisha yao kama kawaida, linaweza kukuumiza sana.

Unachopaswa kujua rafiki ni kwamba, kila mtu anapitia hali ya namna hii kwenye safari yake ya mafanikio. Siyo wewe pekee na siyo kwamba unakosea sana. Ndivyo mambo yanavyokuwa na yanakuwa hivyo kwa kila mtu.

Katika nyakati za aina hii, ndipo wengi huchukua hatua ambazo huwaondoa kabisa kwenye njia ya mafanikio. Kama ni biashara wanaachana nayo na kuona haiwafai, kama ni kazi wanaacha kuendelea kuweka juhudi. Na kwa njia hiyo wanakuwa wamepoteza fursa nzuri ambayo walishaijenga kwa ajili ya mafanikio yao.

SOMA; Mambo Matano (05) Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Wa Kupanga Bei Ya Huduma Au Bidhaa Kwenye Biashara Yako.

Njia pekee ya kushinda hali hii, ni kutengeneza mfumo wako wa safari ya mafanikio, kisha kwenda na mfumo huo. Mfumo huu utaongozwa na ndoto kubwa ya maisha yako, utakuelekeza hatua zipi unapaswa kuchukua. Kwa kufuata mfumo huu, utaendelea kuchukua hatua hata kama mambo yanaonekana yamesimama. Na hivyo pekee ndiyo unaweza kuyasukuma kwenda mbele.

Hakuna siku umelala ukawa na wasiwasi asubuhi haitafika, hata kama giza ni nene kiasi gani, tunajua baada ya muda fulani, giza litaisha na kutakucha tena. Ni mfuko unaoenda hivyo kila siku. Hivi pia ndivyo inapaswa kuwa kwenye maisha yako ya mafanikio. Kwa kuendelea kuweka juhudi, hata kama mambo yanaonekana kukwama sasa, una uhakika yatanyooka na kwenda vizuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.