UKURASA WA 910; Ndiyo, Lazima Upoteze…

By | June 28, 2017

Unajua kwa nini watu wengi wanaogopa kufanya mabadiliko kwenye maisha yao?

Kwa sababu mabadiliko ya aina yoyote ile, yanahusisha kupoteza, kwenye kila mabadiliko kuna vitu unavyovipenda ambavyo utavipoteza, na hilo wengi hawapendi kulikaribisha.

Ninachokuambia hapa leo ni kwamba lazima upoteze, kama unataka kutoka hapo ulipo sasa na kupiga hatua zaidi.

Lazima kuna watu ambao utahitaji kuwapoteza kwenye maisha yako, siyo kuwaua, la hasha, ila kuachana nao, kutokutumia muda wako na wao, au kuacha kufanya mambo ambayo ulikuwa unafanya nao. Sasa kama watu hawa wanakuuma sana kuwaacha, utaendelea kubaki hapo ulipo.

Lazima kuna vitu unapenda kufanya sasa, ambavyo lazima uvipoteze, lazima uache kuvifanya. Kwa sababu huwezi kuendelea kuvifanya na kuweza kufanya makubwa pia. Utahitaji kuacha vitu hivyo unavyopenda sana, lakini havina mchango kwenye mafanikio yako.

SOMA; Sababu Za Kijinga Zinazokupotezea Wateja Kwenye Biashara Yako.

Lazima kuna fedha itabidi upoteze ili uweze kupata fedha zaidi. Ndiyo, japo unachotaka ni fedha, lakini hutazipata mpaka uwe umepoteza fedha kiasi. Hii inawezekana ni kuacha baadhi ya vitu unafanya sasa, ambavyo vinakupa kipato kidogo, na kuanza kufanya vitu vingine ambavyo vinakupa kipato kikubwa. Hivyo mwanzoni utapoteza kipato kidogo, kutengeneza kipato kikubwa zaidi.

Upo usemi kwamba huwezi kula keko yako na ukabaki nayo. Usemi huu una ukweli sana, kwamba kama unataka keki kubwa, inabidi ule kwanza keki ndogo uliyonayo. Halafu upate hamasa ya kutoka na kwenda kutafuta keki kubwa zaidi.

Kuwa tayari kupoteza, mabadiliko yoyote yanahusisha kupoteza kitu, mafanikio yoyote yanakuja kwa gharama. Usitake kubaki kama ulivyo sasa, lakini upate mafanikio makubwa. Ni kujidanganya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.