UKURASA WA 923; Anayekutawala Anakunyima Vitu Hivi Vitatu…

By | July 11, 2017

Kwenye hii dunia, wapo watu wengi sana ambao wanajaribu kukutawala, ili waweze kukutumia kwa madhumuni yao binafsi bila ya kujali wewe unataka nini. Na ili wafanikiwe kukutawala, wanahakikisha wanakunyang’anya au kukunyima vitu vitatu muhimu. Ukishavikosa vitu hivi tu, huna tena ujanja, lazima utakaa chini ya anayekutawala na hutakua na namna ya kujinasua.

Kitu cha kwanza anachokunyima ni kujiamini.

Anayekutawala anahakikisha kwa namna yoyote ile hujiamini. Huamini kama unaweza kufanya wewe mwenyewe au nje ya mtawala wako. Unaamini ni mtawala wako pekee anayekuwezesha wewe kuweza kufanya unachofanya au hata kuishi. Maisha nje ya mtawala yako yanakuwa ya kutisha na ambayo hayawezekani.

SOMA; Angusha Na Tawala Watu Hawa Wawili Ili Uweze Kuwa Na Mafanikio Makubwa.

Kitu cha pili anachokunyima ni rasilimali.

Mtawala anajua, ukiwa na rasilimali, utaweza kufanya mwenyewe na hivyo kutokumtegemea. Hivyo anachofanya ni kuhakikisha anakunyima rasilimali, ili ushindwe kufanya chochote unachotaka kufanya. Ukishakosa rasilimali za kufanya, huna namna ila kumtegemea mtawala. Rasilimali inaweza kuwa muda, fedha na hata miundo mbinu mingine.

Kitu cha tatu anachokunyima ni watu wa kukuhamasisha.

Mtawala anahakikia huna mtu unayemwangalia, ambaye anakuhamasisha ili uweze kufanya au kuwa kama mtu huyo. Na kwa njia hii mtawala anahakikisha unamwona yeye pekee ndiye anayeweza, wengine wote hakuna wanachoweza na hivyo huna cha kujifunza kwao.

Hivi ni vitu vitatu ambavyo mtu yeyote anayekutawala anakunyang’anya. Anaweza kuwa mwajiri wako, anaweza kuwa mshindani wako kibiashara, anaweza kuwa kiongozi wako kijamii au hata kidini na anaweza kuwa mwenza wako.

Cha kusikitisha zaidi, unaweza kutumia mambo hayo matatu kujishusha wewe mwenyewe. Ikawa hakuna mtawala ila huwezi kupiga hatua kwa sababu unajidharau, hutafuti rasilimali za kutumia na pia huna watu waliofanikiwa ambao unawaangalia kama sehemu ya kuhamasika zaidi.

Hakikisha kila wakati unakuwa na vitu hivyo vitatu, vitakuwezesha kupiga hatua kubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.