UKURASA WA 926; Hakuna Muda Zaidi…

By | July 14, 2017

Sababu ya kukosa muda ndiyo sababu inayotumiwa na wengi, hasa wanaposhindwa kufanya mambo muhimu kwenye maisha yako. Lakini tukitafakari kwa kina, tunaona wazi kabisa hakuna siku muda utaongezwa. Masaa ni yale yale 24 kwa siku, siku ni zile zile saba kwa wiki na wiki ni zile zile 52 kwa mwaka.

Hii ina maana kwamba kutumia sababu ya muda, ni kutaka kuficha uzembe ambao upo ndani yako. Hutaki kukiri kwamba kuna mambo huzingatii.

Kwa kuwa tunajua hakuna muda zaidi, kulalamikia muda ni kupoteza muda. Badala yake tunahitaji kutengeneza muda. Kama unachosubiri hakiji, si unapaswa kutengeneza chako? Na hapa ndiyo pazuri, tutengeneze muda wa kufanya yale muhimu.

Na siri pekee ya kutengeneza muda ni kuwa na vipaumbele. Kama jambo ni muhimu, tutapata tu muda wa kulifanya, hata kama tumebanwa kiasi gani. Hii ni kwa sababu tunachagua kutengeneza muda wa jambo hilo.

SOMA;  Nunua Muda Kwanza….

Sasa tumia dhana hiyo hiyo katika kutengeneza muda wa mambo mengine muhimu kwenye maisha yako. Hakikisha unaweza kipaumbele wa mambo gani unafanya kwanza kabla ya mengine. Panga ratiba yako ya siku ikiwa na yale muhimu kwanza kabla ya mengine. Kwa sababu ukianza kufanya yale muhimu, unatumia muda wako vizuri. Ila ukianza na yale ambayo siyo ya muhimu, mara zote utaona muda unaenda na hakuna cha maana umefanya.

Hakuna muda zaidi, hivyo ni wajibu wetu kutengeneza muda tunaotaka kwa ajili ya yale muhimu zaidi kwetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.