UKURASA WA 931; Kama Tatizo Halitatuliki…

By | July 19, 2017

Huenda ni njia unayotumia ndiyo inafanya tatizo lishindikane kutatulika.

Kwa sababu ni kawaida kwetu sisi binadamu kupenda kufuata njia rahisi kwenye chochote tunachofanya. Tunaangalia wapi ambapo tunaweza kuweka nguvu kidogo au gharama kidogo ili kupata kile ambacho tunataka.

Lakini matatizo makubwa, yanahitaji zaidi ya kuweka nguvu na gharama kiasi. Yanahitaji ujitoe zaidi ya kawaida, yanabidi uwe tayari kugharamia zaidi.

Chukua mfano wa mtu ambaye ana tatizo la kipato miaka nenda miaka rudi. Kila anapokazana anarudi pale pale, fedha hana na madeni ni mengi. Mwangalie au kama ni wewe jiangalie kwa makini. Angalia namna unafanya kazi au biashara zako, angalia namna unaenda na maisha yako ya kawaida, angalia namna unajitoa.

SOMA; Mambo Matano(05) Ya Kufanya Pale Unapokuwa Umekwama.

Kama huwezi kufanya kazi muda wa ziada, kama huwezi kufanya zaidi ya unavyolipwa, kama huwezi kuchagua kukosa vitu ambavyo kila mtu anafanya lakini siyo muhimu, unafikiri utatokaje kwenye tatizo hilo?

Au mtu anakuambia kila akijaribu biashara anashindwa. Sasa angalia namna anaendesha biashara zake, kwa mazoea, hakuna kujituma, wateja hawajaliwi, hakuna usimamizi, yeyote anayefanya kazi kwenye biashara hiyo anaweza kufanya chochote anachojisikia kufanya.

Kama tatizo linashindikana kutatua, kabla hujasema limeshindikana, hebu kwanza angalia namna unalitatua. Kama unaweka juhudi za kawaida na hupo tayari kuweka gharama kubwa, unapoteza muda wako bure tu, utaendelea kujaribu na kujaribu lakini hutalitatua.

Wakati mwingine unatafuta njia ya mkato ya kutatua tatizo, na unashangaa kukutana na matatizo zaidi. Hapo ndiyo wakati wa kurudi kwenye njia sahihi, njia ndefu na ngumu, ila ya uhakika ya kupata kile unachotaka.

Hakuna tatizo linaloweza kushindikana, iwapo mtu atakuwa tayari kuweka juhudi, nguvu na gharama zinazohitajika kuwekwa. Pia uvumilivu na muda ni vitu muhimu katika kuhakikisha unatatua tatizo linalokusumbua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.