UKURASA WA 941; Juhudi Hizo Weka Kwenye Kila Eneo La Maisha Yako…

By | July 29, 2017

Juhudi kubwa unazoweka katika kuhakikisha unakuwa na kipato cha kutosha, ni juhudi hizo hizo unapaswa kuweka kwenye kuhakikisha mahusiano yako na watu wengine ni bora, afya yako ni bora, imani yako iko vizuri na kila kitu kinachokuhusisha wewe, kinaenda kwa ubora wa hali ya juu.

Huwezi kuwa bora sana kwenye maeneo machache ya maisha yako, maeneo mengine ukawa hovyo halafu bado ukayafurahia maisha yako, haitatokea.

Hata kama utakuwa na fedha nyingi kiasi gani, kama huna mahusiano mazuri na familia yako, kama afya yako ni mbovu na kama huna mchango unaoona unatoa kwa wengine, utaona maisha yako hayana maana.

Ndiyo maana nimekuwa nakushauri sana kwamba kila eneo la maisha yako, weka juhudi kubwa, nenda hatua ya ziada. Hakuna eneo ambalo siyo muhimu, hivyo weka juhudi kubwa kwenye kila eneo.

Eneo lolote la maisha yako ambalo hutaweka juhudi na likawa na udhaifu, jua hilo ndiyo eneo ambalo litakurudisha nyuma kwenye maisha yako. Hata kama utapiga hatua kubwa kiasi gani kwenye maeneo mengine, kama eneo moja utakuwa nyuma, maisha yako yataonekana bado hayajakamilika.

SOMA;  Huenda Tatizo Siyo Juhudi…

Yasimamie maeneo makuu ya maisha yako, afya, mahusiano, imani, fedha na kazi/biashara. Hakikisha kila eneo unakuwa bora zaidi kila siku, unaweka juhudi zaidi, unakwenda hatua ya ziada kuhakikisha upo pazuri.

Usilegeze kamba kwenye eneo lolote la maisha yako, litakugharimu zaidi kwenye mafanikio yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.