UKURASA WA 944; Hatua Muhimu Kuchukua Pale Unapozama…

By | August 1, 2017

Kipaumbele cha kwanza kwa mtu anayezama, ni kukazana asizame. Hana kingine ambacho anaruhusu akili yake ifanyie kazi zaidi ya kukazana asizame. Lakini changamoto kubwa kwenye kuzama ni moja, kadiri mtu anavyokazana asizame, ndivyo anavyozidi kuzama. Kadiri mtu anatapatapa asizame, ndivyo anavyozidi kuchoka na kuendelea kuzama.

Hivyo usitegemee jambo lolote kubwa kwa mtu anayezama. Kwa sababu akili yake ipo kwenye kutokuzama na hawezi kujali kitu kingine zaidi ya kile.

Kuzama kwenye maisha, ni jambo lolote linalotokea, ambalo linatufanya tushindwe kuendelea na maisha yetu ya kila siku. Kwa mfano kama upo kwenye madeni makubwa, unazama. Kama upo kwenye changamoto za kimahusiano unazama. Kama upo kwenye changamoto ya kipato unazama.

Tatizo kubwa la kwenye kuzama ni zile hatua ambazo mtu anachukua ili asizame. Badala ya kumwokoa asizame, zinazidi kumzamisha zaidi. Na hilo linakuwa hatari zaidi kwenye maisha yake.

SOMA; Hatua Kubwa Kubwa…

Hivyo basi, wakati wowote unapojikuta unazama, pale mambo yanapokwenda tofauti na unavyotaka, kabla hujakimbilia kuchukua hatua, kwanza kaa chini na ujue chanzo halisi ni kipi. Kabla hujakimbilia kujiokoa usizame, ni vyema kujua kipi kimekufikisha pale ulipo kwa sasa.

Kwa mfano kama kinachokuzamisha ni madeni, ni rahisi kukimbilia kukopa ili kulipa deni, lakini hilo halisaidii, badala yake linatengeneza tatizo kubwa zaidi. Tatizo la msingi linakuwa ni kukosa nidhamu ya fedha na hivyo bila ya kujijengea nidhamu hiyo, hakuna namna unaweza kuondoka kwenye kuzama huko.

Kadhalika kwenye changamoto na migogoro mingi. Ni rahisi kulaumu wengine na kuona wao ndiyo wenye matatizo na wanapaswa kubadilika, lakini hilo linapelekea hali kuwa mbaya zaidi, kwa sababu ukiwarushia wengine lawama, wanachokimbilia kufanya ni kukana lawama hizo na kujitetea. Hivyo hatua sahihi ni kuona wewe binafsi umechangiaje kwenye hali hiyo. Na kuwa tayari kubadilika wewe.

Unapokuwa unazama kwenye maisha, kwenye mambo mbalimbali, usikimbilie kupiga mbizi kuondoka kwenye kuzama huko, bali jua kipi hasa kimekufikisha pale na chukua hatua sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 944; Hatua Muhimu Kuchukua Pale Unapozama…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.