UKURASA WA 949; Kitu Pekee Muhimu Sana Kwenye Maisha Yetu Ya Mafanikio…

By | August 6, 2017

Ni mahusiano bora.

Ndiyo maana wale wote ambao wanakazana kupata vitu bila ya kujali watu, huishia kupata vitu hivyo lakini wanakuwa na upweke mkubwa ndani yao.

Mahusiano bora ndiyo kitu pekee muhimu sana kwa mafanikio yetu, kuanzia kwenye kazi au biashara, na hata kwenye maisha yetu ya kawaida. Pale mahusiano yetu yanapokuwa bora, mafanikio yetu yanakuwa na maana.

Mahusiano mazuri ni hitaji la msingi la kila binadamu, kwa sababu ndiyo asili yetu. Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa tunaishi pamoja, kama familia, koo, jamii na hata falme.

Kitu pekee ambacho kimewezesha jamii yetu binadamu kuendelea kuwepo hapa duniani, ni kuwa karibu, kuwa na mahusiano mazuri, ambayo yanapelekea kusaidiana na kuwa salama pamoja.

Katika kujenga mahusiano mazuri kwako, kaa na wale watu ambao unawapenda, na jali kuhusu wao.

SOMA;  Sisi Ni Bora Kuliko Wao, Uongo Tunaojidanganya Mara Zote Na Kuharibu Mahusiano Yetu Ya Kijamii.

Kuanzia kwenye familia, pata muda wa kukaa na watu muhimu kwenye maisha yako, wapate muda wako na kujali kwako. Hii itatengeneza maisha mazuri na yenye ushirikiano mkubwa.

Kwenye kazi na biashara pia, chagua kuzungukwa na watu ambao unawapenda na wanakupenda, watu ambao mnajaliana, na kazi au biashara itakuwa bora sana kwako. Lakini kama utazungukwa na watu wasiokupenda, wasiojali kuhusu wewe, kazi au biashara yako itakuwa chungu kwako. Hata kama unatengeneza kiasi kikubwa sana cha fedha, kila ukifikiria kazi au biashara hiyo, hupati kabisa hamasa ya kwenda.

Jali zaidi mahusiano, kwa kila nafasi unayoipata, jenga mahusiano bora, haya ndiyo yanaleta mafanikio na ndiyo yanafanya mafanikio yetu kuwa na maana kwetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.