UKURASA WA 955; Zawadi Kubwa Unayoweza Kumpa Mtu Kwenye Zama Hizi…

By | August 12, 2017

Tunaishi kwenye kipindi ambacho changamoto zipo nyingi na zinazidi kuwa nyingi kadiri siku zinavyokwenda. Usumbufu ni mwingi na kelele ni nyingi kiasi kwamba kila mtu anakuwa kama amevurugwa, asijue afanye lipi na aache lipi. Au amsikilize nani na kumpuuza nani.

Hili limepelekea zawadi kubwa sana ambayo unaweza kumpa mtu zama hizi kuwa MUDA NA USIKIVU.

Muda umekuwa adimu sana, kila siku mambo ya kufanya yanaongezeka, lakini muda ni ule ule. Kila mtu ni kama anakimbizana na kitu kila wakati. Ni vigumu sana kukuta mtu kwa wakati wowote hana cha kufanya. Kwani hata kazi ikiisha, simu inashika nafasi yake. Kwa kifupi, watu hawana muda kabisa.

Usikivu umekuwa changamoto zaidi kwenye zama hizi. Watu wapo sehemu moja, lakini mawazo yao yapo sehemu nyingine kabisa. Siku hizi hata watu wakitembeleana, baada ya salamu, kila mtu anazama kwenye simu yake. Wapo eneo moja lakini kila mtu akili na mawazo yake vipo mbali kabisa, kwenye mtandao wa intaneti.

Kwa changamoto hiyo ya muda na usikivu, inakuwa zawadi kubwa sana unayoweza kumpa mtu. Kwa sababu kila mtu anahitaji muda wa mwingine, na kila mtu anataka kusikilizwa na wengine. Wewe ukijua ni watu gani wanastahili muda na usikivu wako, utaweza kutengeneza mahusiano bora sana yatakayokuletea mafanikio makubwa.

Kwenye kazi/ajira.

Kwenye kazi, hili ni muhimu mno, kwa sababu kila mtu hana muda na hakuna usikivu. Hivyo ukipanga muda wako vizuri, wa namna gani unatekeleza majukumu yako ya kazi, na ukasimamia mpango wako huo vizuri, utaweza kumaliza kila kazi kwa muda wake na hutakuja kukumbushwa kwamba tarehe ya mwisho imefika.

Pia unapokuwa msikivu, unaelewa vizuri majukumu ya kazi, kutoka kwa mwajiri wako au kwa wale ambao unafanya nao kazi. Kwa kuwa msikivu, utajua nini kinahitajika na unawezaje kukitoa kama kinavyohitajika.

SOMA; Zawadi Kubwa Kabisa Unayoweza Kumpa Mteja Wako.

Kwenye biashara.

Hakuna eneo ambalo muda na usikivu vinahitajika kama kwenye biashara. Kwa sababu watu hawana muda, wamekuwa hawajali sana wateja wao, hivyo wewe ukitenga muda wa kuwahudumia vizuri wateja wako, kwa kuwapa muda, watakuthamini sana.

Pia usikivu umekuwa mdogo kwenye biashara, mteja ana mahitaji na maumivu ambayo kama ukimsikiliza utaweza kumsaidia vizuri na akawa mteja wako wa kudumu. Lakini huwezi kupata nafasi hiyo iwapo utakuwa unatumia simu wakati mteja anakueleza mahitaji yake. Hata kama umezoea biashara yako kiasi gani, hilo linakuondolea usikivu na mteja ataona haupo pamoja naye.

Hivyo kwenye biashara yako, mpe mteja muda, na msikilize kwa makini, ujue maumivu yake na mahitaji yake, kisha mpe kile ambacho kitamsaidia kweli.

Kwenye maisha kwa ujumla.

Kila mahali ambapo unakutana na watu wengine, iwe familia, marafiki na wengine, utaboresha zaidi mahusiano yako iwapo utatenga muda wa kuwa na watu hao, na pia utakuwa msikivu.

Tenga muda wa kukaa na wale watu ambao unawajali, wale ambao ni wa muhimu kwako. Na hili litaboresha mahusiano yenu na kufanya maisha kuwa bora.

Pia kuwa msikivu pale ambapo mtu anakueleza jambo lolote ambalo ni muhimu kwake. Usioneshe tu kwamba unasikiliza, bali kuwa pamoja naye. Mara nyingi watu wana matatizo makubwa kwenye maisha yao kwa sababu tu hawajapata watu wa kuwasikiliza. Wakati mwingine kumsikiliza tu mtu kunampunguzia mzigo, hata kama hutamsaidia au kumshauri lolote, kwa wewe tu kuchukua muda na kumsikiliza, anajisikia kutua mzigo mkubwa kwake.

Kwa kuwa muda ni mchache na huwezi kufanya kila kitu, lazima uchague sana nani utampa muda wako na nani utamsikiliza. Fanya hivyo kwa wale wanaostahili kupata muda na usikivu wako, wale ambao wanajali kile unachofanya na kujali kuhusu wewe. Ndiyo maana pia ni muhimu kwenye kazi na biashara, ufanye na watu ambao unawapenda na kuwajali. Tofauti na hapo, hutasukumwa kutenga muda au kuwasikiliza.

Wape watu muda, wasikilize, utajifunza mengi na utaboresha mahusiano yako kwenye kila eneo la maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.