UKURASA WA 956; Usijioneshe, Bali Onekana…

By | August 13, 2017

Mtu mmoja amewahi kunukuliwa akisema watu huingia kwenye matatizo pale wanapotumia fedha ambazo hawana, kununua vitu ambavyo hawavihitaji ili kuwaridhisha watu ambao hawajali.

Umeliona mara ngapi hilo? Labda kama hujaelewa vizuri hapo kwenye huo usemi, ni kwamba watu wengi wamekuwa wanakopa vitu ili kujionesha kwa wengine kwamba na wao wana vitu hivyo, halafu watu wenyewe wanaowataka waone, wala hata hawajali kiasi hicho.

Mtu mwingine amewahi kunukuliwa akisema unaweza kuwa tajiri au kujionesha kwamba ni tajiri. Akieleza kwamba, watu wengi ambao kwa nje wanajionesha wana utajiri huwa hawana. Na wale matajiri halisi, huwezi hata kuwadhania, maisha yao yanakuwa kawaida sana.

Rafiki, kwenye ukurasa wa leo nataka tuingie ndani kabisa kwenye hili, ili kuhakikisha haliingilii mipango yetu ya maisha ya mafanikio.

Ni hitaji letu sisi kama binadamu kutaka kukubalika na wengine, kupenda kuonekana ni wa muhimu, hakuna ambaye hapendi hilo. Ndiyo maana watu wanavaa nguo nzuri, zenye mwonekano mzuri, watu wanajiremba au kuwa watanashati. Yote hayo ni kutaka mwonekano wetu mbele ya wengine uwe mzuri na watukubali.

Na hili siyo tu kwa ajili ya kuonekana, bali pia kwa ajili ya kazi na biashara pia. Huwezi kufanya kazi au biashara na watu kama huonekani vizuri. Mwonekano wako kwa mara ya kwanza ndiyo kinawashawishi watu kufanya kazi na wewe. Kadhalika kwenye mahusiano yetu na wengine, mwonekano wetu unahusika.

SOMA; Ukuta Usioonekana…

Lakini sasa, tusiende zaidi kwenye hili, tusikazane kujionesha kwa vitu ambavyo havina maana kwetu. Ukishakuwa na yale mahitaji ya msingi kama binadamu, basi weka mkazo kwenye vile vitu ambavyo ni muhimu kwako na siyo kutaka kujionesha.

Usiingie gharama kubwa ambazo huna, au ambazo ungeweza kuzipeleka sehemu yenye manufaa, kwa sababu tu unataka kuwa na kitu fulani ambacho wengine wakikuona nacho watakukubali. Hili siyo tu kwamba linakupotezea fedha, bali pia litakuangusha kwa sababu utakuja kugundua watu wala hawajali kama ulivyokuwa unafikiria. Utaona una kile kitu, halafu hakuna hata anayekuchukulia kwa hali ya juu kama ulivyofikiri.

Ndiyo maana leo nakuambia kitu kimoja, usijioneshe, bali onekana.

Hapa utaniuliza tofauti ya kujionesha na kuonekana ni ipi?

Kujionesha ni pale ambapo unafanya kitu ambacho siyo muhimu kwako na wala hukijali, ila tu unafanya kwa ajili ya kuonekana na wengine. Unaingia gharama kubwa ili tu kuwaridhisha wengine.

Kuonekana ni pale unapofanya kitu ambacho unajali, kitu ambacho ni muhimu kwako, halafu unawapa wengine fursa ya kuona hilo. Hapa unawasaidia kuweza kupata kile unachotoa na pia unawapa hamasa kwamba inawezekana.

Usipende kuwa mtu wa kuonekana kwa vitu, bali kuwa mtu wa kujulikana kupitia vile unavyofanya. Julikana kwa kazi au biashara unayofanya, julikana kwa namna unavyojituma kwenye kile unachofanya na pia julikana kwa tabia ulizojijengea, uaminifu, uadilifu, uchapakazi na kuwasaidia wengine.

Kwa njia hii utaweza kupiga hatua kubwa, kwa sababu kile unachofanya kina maana kwako na utaendelea kuwa na hamasa ya kufanya, hasa pale wengine wanapokutegemea kupitia kile unachofanya. Kwa mfano kama watu wanakujua kama mfanyabiashara ambaye muda wote unaweza kutegemewa kutoa bidhaa au huduma bora, basi utakazana kuhakikisha hadithi hiyo inaendelea kuwa hivyo. Hapo umeonekana na kujulikana kwa kile ambacho ni halisi kwako, na siyo maigizo.

Kamwe usiishi maisha ya kuigiza, ukishapata yale mahitaji ya msingi kwako, mkazo mkubwa weka kwenye yale ambayo ni muhimu kwako.

Na mwisho kabisa, sisemi usiwe na vitu vizuri ambavyo wengine wanaweza kukuona na wewe upo, ninachosema ni uwe na vipaumbele. Kwa kweli ukienda kukopa gari zuri ili tu uonekane na wewe una uwezo, hakuna yeyote ambaye unamdanganya ila wewe mwenyewe. Lakini kama umeshafikia uhuru wa kifedha, una biashara zinazojiendesha kwa faida, una uwekezaji unaokuzalishia, na unapenda kuwa na gari zuri kuliko wengine wote, ambalo lipo ndani ya uwezo wako, hakuna wa kukuzuia kuwa na gari ya aina hiyo utakayo wewe.

Usijioneshe, onekana, kwa kuweka vipaumbele kwenye mambo ambayo ni muhimu na yana maana kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

2 thoughts on “UKURASA WA 956; Usijioneshe, Bali Onekana…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.