UKURASA WA 957; Ongea Unavyotaka, Lakini Watu Watasikia Wanachotaka Kusikia…

By | August 14, 2017

Moja ya eneo lenye changamoto kubwa sana kwenye maisha yetu ni mawasiliano. Unaweza kuongea kitu kwa nia njema kabisa, lakini wengine wakatafsiri kuwa cha nia mbaya na ukaonekana wewe ni mbaya.

Hii ni hali ya kawaida kabisa, hivyo kabla hujalalamika au kujitetea kwenye hilo, unapaswa kwanza kulielewa kwa undani.

Watu hawasikii kile kinachosemwa, bali wanasikia kile ambacho wao wanataka kusikia. Hii ikiwa na maana kwamba, mtazamo ambao watu wanao juu ya kitu fulani, unaathiri namna wanavyopokea kile ambacho wanaambiwa.

Na hii ndiyo sababu mara zote ukisikia kitu kwa mtu, ukienda kumuuliza mtu uliyeambiwa amesema, atakuambia hakusema hivyo, mara zote, wewe jaribu tu kwenye jambo lolote. Huenda kuna kitu kitakuwa kimeongezwa, kimepunguzwa au kimebadilishwa maana.

Watu wakishakuwa na mtazamo fulani, basi kila wanachosikia, watakitafsiri kulingana na mtazamo ambao tayari wanao.  Kama mtazamo wao ni kwamba yule anayesema ana dharau, basi kila neno watalitafsiri kwa dharau. Iwapo mtazamo wao ni kwamba anayesema ni mwongo, bali kila neno watalitafsiri kama uongo.

SOMA;  Sikiliza Zaidi Ya Unavyoongea…

Ndivyo tulivyo sisi wanadamu, na ndiyo maana kuujua ukweli ni kitu kigumu mno, kwa sababu mitazamo na hisia zetu zinatuzuia sisi kufikiri sawa sawa. Tunakuwa hatuoni au kusikia kitu kama kilivyo, badala yake tunaona na kusikia kile tunachotaka sisi.

Sasa kujua hili kunatusaidia nini sisi?

Moja; kukazana kuvuka hali hiyo kila wakati.

Pale unapomsikiliza mtu, jaribu kuondoa mtazamo wowote ulionao juu ya mtu yule na msikilize yeye kama yeye. Msikilize kile alichosema na hakikisha umemwelewa kwa usahihi. Na kama kuna eneo hujamwelewa unaweza kumuuliza swali au kumwelezea ulivyoelewa ili akuambie ndivyo au sivyo.

Hili ni muhimu sana kwenye yale maeneo muhimu ya maisha yako kama kazi, biashara na hata mahusiano na watu wa karibu. Kwa sababu unaweza kuwa hukusikia vizuri kitu, ukaondoka na ujumbe ambao siyo sahihi na kuishia kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri.

Mbili; hakikisha watu wamekuelewa kwa kile unachowaambia.

Pale unapotoa ujumbe, hasa ujumbe ambao ni muhimu sana, hakikisha wale wanapokea ujumbe huo wamekuelewa. Katika kuhakikisha hilo kwamba umeeleweka, uliza maswali na pia waulize watu wameelewaje.

Kwa kuuliza maswali utapika kiasi cha uelewa kwa watu na kwa kuwataka wakuambie wameelewaje ulichowaambia, itakuonesha kama ujumbe uliopokelewa ndiyo ujumbe sahihi.

Hivyo unaweza kumwuliza mtu umeelewaje kwenye hili nililosema? Na yeye akakushirikisha kile alichoelewa.

Kama huwezi kuuliza uelewa wao, basi unaweza kuwaangalia hatua wanazochukua, angalia kwa makini na ona kama ulichoeleza kimeeleweka. Kama unaona watu wanavyofanya ni tofauti na ulivyosema, unahitaji kuwapa maelezo sahihi kuhakikisha wameelewa.

Tatu; kamwe usikubali kwa asilimia 100 maneno ya kusikia.

Mtu akija kwako, akakuambia fulani alisema hivi na hivi, usibebe maneno yote hayo na kuyaamini kwa asilimia mia moja. Hata kama ni mambo mazuri unaambiwa. Jua kwamba kuna ambayo yatakuwa yamesahaulika, yapo yaliyoongezwa na yapo ambayo yamebadilishwa maana.

Kama hujamsikia mtu wewe mwenyewe kwa masikio yako akiongea, au kusikia sauti yake iliyorekodiwa, basi kile unachosikia kwa wengine siyo sahihi kwa asilimia mia moja.

Kamwe usifanye maamuzi makubwa kwa maelezo ya kusikia kutoka kwa wengine, kama unayo nafasi, hakikisha unasikia wewe mwenyewe moja kwa moja ndiyo uweze kufanya maamuzi.

Kile unachoongea siyo kile watu wanasikia, hivyo kuwa makini na unachosikia na hakikisha watu wanaelewa kile unachoongea.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

3 thoughts on “UKURASA WA 957; Ongea Unavyotaka, Lakini Watu Watasikia Wanachotaka Kusikia…

  1. Deodatus

    AsaNte kocha kwa ujumbe mzuri kila habari niNayoipokea kupitia mtu mwingine asiye mhusika mkuu kuna maneno YALIYO SAHAULIKA, YALIOONGEZWA na pia KUBADEILISHWAA MANAA

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.