UKURASA WA 958; Kesho Inapuuza Vitu Hivi Viwili…

By | August 15, 2017

Kila mtu ana hisia na maoni yake juu ya jambo lolote lile. Ndiyo maana huwa hakitokei kitu watu wakakosa la kusema na kuhisi pia.

Watu watajigawa wenyewe, wale ambao watakubaliana na kitu, kukisifia na kutafuta kila ushahidi wa kuonesha kwamba kitu kile ni sahihi na kweli kabisa. Kuonesha kwamba ndiyo kitu kinachopaswa kufanywa na kila mtu.

SOMA; Usiitabiri Kesho Yako, Bali Itengeneze…

Upande wa pili watakuwepo wale ambao wanaona ni kitu kibaya hakifai, au yapo makosa ambayo yanafanyika kwenye kitu hicho. Watakuwa na ushahidi kabisa wa kuonesha kwa nini ni kitu kibaya au hakifai au kina makosa.

Lakini kesho inapuuza wote, kwa hisia na maoni yao. Kesho inaangalia misingi ambayo kitu kimejengwa, kesho ina mabadiliko, siyo sawa na leo.

Hivyo basi, yeyote anayeongea leo, huenda anapoteza muda wake, kwa sababu siku siyo nyingi, maoni anayotoa leo hayatakuwa na maana tena. Mambo yatakuwa yamebadilika sana, vitu vitakuwa tofauti kabisa.

Muda ni mwalimu mzuri, kwa sababu unajua kumfundisha kila ambaye anafikiri anajua sana au yupo sahihi sana. kwa sababu wengi hawana subira, na kila anayetabiri lolote anakosea, muda hutoa funzo kubwa.

Muda pia ni tabibu mzuri, haijalishi kitu gani kimetokea leo, baada ya muda mambo yatakuwa mazuri, watu watakubali kuishi na hali iliyotokea, au hali itakuwa bora. kwa vyovyote vile, kesho haitakuwa kama ilivyo leo. Mvua zitanyesha tena, jua litawaka tena, nyasi zitaota tena na majira mapya yatakuja. Hakuna kitakachobaki kama kilivyo leo, haijalishi watu wanatabiri kwa kiasi gani.

Hivyo basi rafiki,

Ni vyema ukaokoa muda wako, kwa kuachana kabisa na utabiri wa aina yoyote kuhusu mambo yajayo. Sisi binadamu ni wabovu sana kwenye utabiri, hakuna mtu awezaye kutabiri kwa uhakika wa asilimia 100, wapo ambao wanabahatisha mara chache, lakini hakuna ambaye ameweza kufanya kwa uhakika mara zote.

Utakuwa sahihi kama utawapuuza wale wanaosema mambo yatakuwa mabaya zaidi, na niamini kwenye hilo. Kwa sababu akili zetu binadamu zina tabia ya kutafuta tatizo, mambo yakiwa mazuri tunaangalia wapi pana upungufu, wapi penye tatizo, na huwa hatukosi tatizo hilo. Hivyo mabadiliko yoyote yanayotokea leo, watu hutabiri kwamba mambo yatazidi kuwa mabaya. Huenda kweli yakawa mabaya, lakini unajua nini? Wewe utakuwa bora zaidi kesho kuliko ulivyo leo, kwa sababu leo umejifunza.

Mabadiliko yanatokea na yataendelea kutokea, kutamani mambo yarudi kama zamani ni kujidanganya tu, hilo halitatokea. Hivyo badala ya kupambana na mabadiliko yanayoendelea, utakuwa mjanja kama utayapokea haraka na kwenda nayo vizuri. Au ukiwa mbele ya mabadiliko, mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa upande wako.

Ni bora ukafanya kitu, kuliko kuishia kuongea pekee. Kila mtu anaweza kuongea, kila mtu anaweza kusema naweza kufanya hicho, lakini ni wachache sana wanaoweza kusema… angalia, nimefanya hichi… hasa pale mambo yanapokuwa magumu, uwezekano wa kushindwa unapokuwa mkubwa na hakuna zawadi yoyote kwenye kufanya.

Kesho ipo kwa sababu ipo, haipo kutimiza hisia zako na maoni yako, kesho itakuwepo kama itakavyokuja, kesho itakupuuza kwa chochote unachotegemea kitokee. Hivyo fanya kile unachoweza kufanya kwa ubora sana leo, kesho itakuja, na kuwa tayari kufanya kilicho bora zaidi kesho. Kuwa na ndoto na maono makubwa, na kuwa tayari kuiishi kila siku kama inavyokuja, kwa kujitahidi kuifanya kuwa bora badala ya kutaka siku iwe bora.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.