UKURASA WA 961; Utakapoanza Kufanya Kitu Hichi Kimoja, Utakaribisha Maadui Wengi…

By | August 18, 2017

Mtu mmoja amewahi kunukuliwa akisema ukitaka watu wasikusumbue kwenye hii dunia, usiseme lolote, usifanye lolote na usiwe yeyote kwenye maisha yako. Kwa lugha nyingine rahisi ni uwepo tu kama wengine walivyo, usionekane na tofauti yoyote ile.

Na hivyo ndivyo uhalisia wa maisha ulivyo.

Unaweza kuwa unafanya kazi, labda umeajiriwa, unafanya majukumu yako kwa ukawaida, kama wengine wanavyofanya, na tabia zako ni sawa kabisa na za wengine, hapo kila mtu anakuwa anakufurahia. Kila mtu anaona wewe ni mtu mzuri na huna shida yoyote.

Lakini siku moja ukaamua hapana, maisha yako hayawezi kwenda hivyo na ukaamua kuweka juhudi kubwa kwenye kazi unayofanya, ukaamua uwe na tabia nzuri na za kipekee, utaibua maadui wa kila aina. Wapo ambao wataona unafanya hivyo kwa sababu unataka kupandishwa cheo, wengine wataona unataka uonekane wewe ni bora zaidi ya wengine. Na hata aliyeko juu yako, atakuona wewe kama hatari kwenye nafasi yake.

SOMA; Maadui Wakubwa Wawili (02) Wa Furaha Kwenye Maisha Yetu.

Kwa kuamua tu kuwa bora, unakuwa umekaribisha uadui wa watu wengi, wote wakipinga hatua mpya na kubwa ambazo unapiga. Kwa sababu hatua zako wewe zinakuwa hatari kwao, kwa sababu wanataka kuendelea kuwa kawaida.

Hii inatokea kwenye kila eneo la maisha yetu, kwenye biashara lipo sana tu, hasa pale unapochagua kuifanya biashara kwa utofauti, au kufanya biashara ambayo haijazoeleka. Wakati mwingine kitendo tu cha wewe kuanza biashara, kitawanyima watu raha na watatengeneza uadui na wewe.

Pale utakapoanza kufanyia kazi ndoto kubwa za maisha yako, hivyo ndiyo siku watu wengi wataibuka na kuwa maadui zako. Wataanza kukuambia namna gani ndoto ulizonazo siyo sahihi, kama vile wanakujua wewe ndani yako una nini. Watakuonesha kwa mifano kwa nini utashindwa.

Utakapoanza kubadilika kwenye maisha yako, labda kuna tabia fulani umekuwa nazo, lakini umegundua zinakurudisha nyuma, ukianza kujenga tabia hizo mpya na zenye manufaa, utakutana na upinzani wa kila aina. Wale waliozoea kuwa na wewe kwenye tabia unayopanga kuiacha, hawatakuacha kirahisi, watataka uendelee kuwa nao zaidi.

Ni muhimu sana kujua na kulielewa hili mapema kabisa kwenye safari yako ya mafanikio, kwa sababu unaweza kuona kama watu hawakupendi na wanakuombea ushindwe. Kumbe yale wanayofanya watu siyo kwa ajili yako, bali kwa ajili yao wenyewe.

Mtu anapokuchukia pale unapochukua hatua kubwa kwenye maisha yako, siyo kwamba chuki zile ni zako, bali chuki zile ni kwao wenyewe, kwa sababu wanajiona wanabaki nyuma. Na binadamu hupata uhakika pale wanapokuwa na wengine, hivyo hata anayepotea, anapenda kutafuta watu ambao atapotea nao. Usikubali kupotekea kwenye maisha ya wengine kwa kufikiri wao ndiyo wapo sahihi zaidi.

Kila mtu atakuwa na maoni juu ya jambo fulani unalochagua kufanya, lakini ukweli wake upo ndani yako wewe. Penda kusikiliza zaidi ukweli uliopo ndani yako na siyo yale maoni ambayo yanatolewa na kila mtu. Wakati mwingine anayekupa maoni ni mtu ambaye alishashindwa, na hivyo hataki mwingine afanikiwe kwa sababu mwingine akifanikiwa basi yeye ataonekana ni mzembe.

Ukiendelea kufanya kila ambacho umezoea kufanya, hakuna atakayehangaika na wewe, hakuna atakayekufikiria wala kuona una hatari kwao. Lakini pale tu utakapochagua kufanya kitu kikubwa na cha tofauti, hapo ndipo utasikia kila aina ya upingamizi na kukatishwa tamaa. Kwa kuwa upo kwenye safari ya mafanikio, lijue hili daima.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

2 thoughts on “UKURASA WA 961; Utakapoanza Kufanya Kitu Hichi Kimoja, Utakaribisha Maadui Wengi…

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.