UKURASA WA 964; Unahitaji Kuongeza Juhudi Kidogo Tu…

By | August 21, 2017

Nikupe siri moja kubwa leo, watu wengi hawaweki juhudi kama ambavyo wanasema au kuonekana wanaweka juhudi. Hii ni kwenye jambo lolote lile ambalo unaona watu wanafanya.

Kwa kifupi watu ni wavivu na wanafanya mambo kwa mazoea. Kila wakati wanaangalia njia rahisi ya kurahisisha lile wanalofanya na kupata muda zaidi wa kupoteza.

Sasa hili ni jambo kubwa na zuri sana kujua kwa sababu, ukiweza kuweka juhudi kidogo tu zaidi ya zile wanazoweka wengine, unayo fursa kubwa sana ya kupiga hatua na kufanikiwa.

Upo mfano wa mafanikio na kupanda ngazi. Kwamba mafanikio ni sawa na kupanda ngazi, au kupanda mlima. Pale chini au kwenye ngazi ya kwanza, huwa panakuwa na watu wengi sana, lakini kadiri unavyopanda juu, watu wanapungua na hali ya hewa inakuwa nzuri sana.

SOMA; Juhudi Hizo Weka Kwenye Kila Eneo La Maisha Yako…

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kuweka juhudi pia, ukiweka juhudi za kawaida, hicho ndiyo kila mtu anafanya, hivyo unapata matokeo ya kawaida, ambayo kila mtu anayapata. Kunakuwa na msongamano mkubwa sana kwenye ukawaida kiasi kwamba hakuna anayekuona.

Lakini unapoanza kuweka juhudi kubwa zaidi ya wengine, unapotoa thamani kubwa zaidi ya wanavyotoa wengine, unaanza kuonekana zaidi ya wengine, unaanza kupanda juu kwenye ngazi ya mafanikio. Ushindani unakuwa mdogo, hali ya hewa inakuwa safi na pia unaona vizuri zaidi ya wale waliopo chini.

Hili ni kwenye kila eneo la maisha yetu.

Kwenye kazi lipo kwenye ufanisi wa kazi, ubunifu, na hata muda ambao mtu anaweka kwenye kazi. Kama umeajiriwa angalia wafanyakazi wenzako wanafanyaje kazi, huenda na wewe upo katikati yao pia. Utaona wengi wanasubiri mpaka waambiwe nini cha kufanya, wakipangiwa cha kufanya mpaka wasimamiwe na kusukumwa. Wanafanya kawaida na muda mwingi wanafanya mambo ambayo hayahusiani na majukumu yao ya kazi.

Vipi kama wewe ukaamua kuyajua majukumu yako vizuri, na ukayatekeleza kabla hata hujakumbushwa, ukaweka ubunifu zaidi na kuboresha kila unachofanya. unamaliza majukumu yako kabla ya wakati unaotegemewa, unawahi kufika eneo lako la kazi kila siku, na hakuna hata siku moja umetoroka au kuondoka kabla ya muda. Unafikiri thamani yako kwenye kazi itakuwa sawa na wengine? Hakika haiwezi kuwa sawa, baada ya muda utakuwa mbali mno, utakuwa umepanda juu zaidi. Na kama siyo hapo ulipo sasa, basi utakuwa upo sehemu nyingine na ukinufaika zaidi.

Kwenye biashara ndiyo kabisa hili lina umuhimu na manufaa makubwa. Wafanyabiashara wengi wanaendesha biashara zao kwa kawaida. Wanaweka bidhaa au huduma, wakisubiri mteja aje. Mteja akija wanamwambia bei na maongezi yanaishia hapo. Wakati mteja anakazana kujua kile anataka kununua kinamsaidiaje, wao wanatumia simu zao. Mteja anachukua hatua ya kulipia kile alichoona kina mfaa, mwishoni anaambiwa hakuna chenchi, hivyo asubiri mpaka itafutwe.

Vipi kama wewe utaingia kwenye biashara, ambapo mteja anapata taarifa zako kabla hata hajakujua, anakuja kwenye biashara yako anapokelewa vizuri, anaelezwa bidhaa na huduma zilizopo, ambazo zitamsaidia kwa tatizo au mahitaji yake. Anauliza maswali na kushauriwa vizuri, anachagua kulipia bidhaa au huduma fulani, anakamilisha, mwisho anapewa zawadi kidogo na kuambiwa karibu tena. Unafikiri mteja huyu ataacha kurudi kwenye biashara yako?

Siri ni ndogo tu, chochote unachofanya, weka juhudi kidogo zaidi ya wengine wanavyoweka, baada ya muda utakuwa mbali kuliko wale wengine wote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.