UKURASA WA 983; Sababu Ya Watu Kutokujali Unachojali Wewe…

By | September 9, 2017

Ushirikiano bora kwenye maisha, kazi na hata biashara, unaanzia kwenye kujali kitu kimoja wote. Yaani wale unaoshirikiana nao, lazima wajali kile unachojali wewe. Au wewe ujali kile wanachojali wao.

Kama unaajiri watu wa kukusaidia, lazima wajali kile unachojali wewe, ili waweze kuchukua hatua unazowataka wachukue.

Kama unachagua watu wa kushirikiana nao kwenye jambo lolote, lazima wajali kile unachojali wewe. Ili kwa pamoja muweze kufanya na kufikia mwafaka wa hatua mnazochukua.

IMG-20170303-WA0001

Lakini changamoto kubwa imekuwa watu kutokujali kile ambacho wewe unajali. Unategemea wafanye kitu fulani na wao wanafanya kitu tofauti kabisa.

Wengi hufikiria kwamba wale ambao hawajali wanachojali wao, ni kwa sababu hawajui wanachojali. Lakini huo siyo ukweli, watu wanajua sana unachojali, kwa sababu wanakuona namna unavyofanya. Hivyo kufanya na kuwaonesha hakutawabadili na waanze kujali.

Sababu pekee inayowafanya watu wasijali unachojali, ni imani. Kama watu hawaamini unachoamini wewe, hawawezi kujali unachojali wewe. Watu wakishapata picha kubwa uliyonayo, wakaiamini picha hiyo kwamba inawezekana, wataanza kujali kile unachojali wewe, kuweka juhudi ambazo unataka waweke ili kupata matokeo bora.

SOMA; UKURASA WA 691; Imani Inayowatenganisha Watu Na Utajiri…UKURASA WA 691; Imani Inayowatenganisha Watu Na Utajiri…

Hivyo unapokuwa na watu ambao hawajali kile unachojali, suluhisho siyo kuwaambia kile unachojali, badala yake kuwafanya waamini kwenye kile unachoamini wewe. Hapa unahitaji kuyatengeneza vizuri maono makubwa uliyonayo, na kujua sababu kubwa ya kufanyia kazi maono hayo, na kwa namna gani yanawezekana, kisha wape watu maono hayo na wafanye waweze kuyaamini.

Imani ina nguvu kubwa ya kuwasukuma watu kuchukua hatua, watu wakishaamini kutoka ndani ya mioyo yao, watakuwa tayari kuweka juhudi kubwa kwa sababu wanajua kwa nini wanafanya vile. Wanaacha kuchukulia kama wajibu pekee na wanaona ni sehemu ya maisha yao kufanya kile wanachopaswa kufanya.

Wafanye watu waamini kile unachoamini na watakuwa tayari kujali kile unachojali wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.