UKURASA WA 987; Ni Kazi Isiyo Ya Kawaida…

By | September 13, 2017

Kuwa mzazi ni jambo la kawaida, kuwa mzazi bora ni kazi.

Kuwa kwenye biashara ni kawaida, kuwa kwenye biashara yenye mafanikio makubwa ni kazi.

Kuwa na shughuli inayokuingizia kipato ni jambo la kawaida, kuwa kwenye shughuli yenye maana kwako, inayokupa kipato ambacho unaweza kukisimamia vizuri ni kazi.

Kuwa mume/mke ni jambo la kawaida, kuwa mume/mke bora sana ni kazi.

Chochote kizuri na bora kwenye maisha, kinahusisha kazi, tena kazi ya maana, siyo ya kawaida.

Hivyo una machaguo mawili kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako, ufanye kawaida kama wengi wanavyofanya, au uweke kazi ili kuweza kufanya tofauti.

Kumbuka ninaposema kazi, namaanisha kazi hasa. Kwa sababu hata wanaofanya kawaida, kuna kiwango cha kawaida cha kazi wanaweka. Sasa mimi kazi ninayokuambia ni kazi kubwa, kazi yenye maana, kazi inayokusukuma kutoka kwenye mazoea.

Jambo

Wapo wengi ambao wanaanza wakiwa na msukumo wa kufanya makubwa, kuwa bora kabisa kwenye kila wanachoanza, iwe ni biashara, ajira, mahusiano n.k. Lakini siku zinavyokwenda, wanazidi kuwa kawaida. Hawa wanakuwa wametekwa na mazoea. Wanaanza kitu vizuri baada ya muda wanafanya kwa mazoea.

Sasa jambo lolote ukishalifanya kwa mazoea, huwezi kuwa bora na huwezi kupata matokeo makubwa na ya tofauti.

Unahitaji kuweka kazi isiyo ya kawaida kwenye jambo lolote unalofanya. Acha kabisa kuwaangalia wengine wanafanya nini, acha kabisa kuangalia jana ulifanya nini.

SOMA; UKURASA WA 911; Maamuzi Ya Mtu Mmoja….

Angalia leo upo wapi, na unataka kufika wapi kisha hatua gani unazoweza kuchukua leo ambazo zitakufikisha kule unakotaka kufika. Na kwa kila hatua unayochukua, angalia ni kitu gani cha tofauti, kipi cha ziada na kipi ambacho hujazoea kufanya, unaweza kufanya kwa siku hiyo.

Iwapo kila siku utaiendea hivi, hakuna kitakachoweza kukuzuia wewe kufanikiwa. Lakini kama utaamua kufanya kawaida, kama ulivyozoea na kama wengine wanavyofanya, usishangae unapopata matokeo ambayo siyo mazuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.