UKURASA WA 989; Weka Nguvu Zako Kwenye Kile Unachoweza Vizuri…

By | September 15, 2017

Unapoanza kufanya kitu chochote kwenye maisha, na kikatoa majibu mazuri, hutakosa watu wa kukushauri ni namna gani unaweza kuboresha zaidi. Watu watakupa mbinu na njia za kuweza kufanya zaidi.

Sasa ushauri na njia nyingi unazopewa huwa zinakuondoa kwenye kusudi lako la mwanzo. Wengi wanaokuwa wanakushauri wanafanya hivyo kwa kuangalia vitu vya nje, kama kupata zaidi au kufika hatua ya juu zaidi.

Ushauri

Lakini huenda wewe ulianza kufanya ukiwa na kusudi la ndani, kwa kuwa ndicho unachoweza kufanya kwa ubora na pia kina maana kwako.

Sasa hapo unahitaji kuwa makini sana kwa sababu utakapoacha ile njia iliyokufanya uanze na kuanza kufuata njia nyingine unazopewa, unaweza kupata kweli yale ya nje, lakini ndani yako usipate kuridhika na kile unachofanya.

Unahitaji kubaki kwenye lile kusudi lako, kufanya kile ambacho kweli kina maana ndani yako. Hichi kitakuwezesha kutoa mchango bora kwa wengine na wewe kuwa bora pia.

Lakini pia unahitaji kufanya yale ambayo uko vizuri katika kufanya, yale unayoweza kuyafanya kwa ubora. Kwa sababu haya ndiyo utatoa majibu mazuri ambayo yatakuwa msaada kwa wengine.

SOMA; Watu Waliofanikiwa Wanasema Uongo, Ndiyo Maana Wengi Wanaojifunza Kutoka Kwao, Hawafanikiwi.

Unapoanza kukimbiza vitu ambavyo siyo vya kwako na havipo kwenye kusudi lako, unapoteza vile vitu ambavyo ni vya kwako.

Weka nguvu zako zote kwenye vile vitu ambavyo vina maana kwako na unaweza kuvifanya vizuri, waache wengine nao wafanye vile wanavyoweza kufanya vizuri na vyenye maana kwao. Usikimbilie kufanya kila kitu kwa sababu unaona wengine nao wanafanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.