UKURASA WA 1006; Kutaka Kupata Na Kuepuka Kupoteza…

By | October 2, 2017

Maamuzi yote tunayofanya binadamu, yanaongozwa na hisia hizi kuu mbili, TAMAA na MAUMIVU.

Tunafanya maamuzi kwa sababu tunatamani kupata kitu fulani, au tunakwepa kupata maumivu fulani.

Lakini katika hisia hizo mbili, ipo yenye nguvu zaidi, ambayo ni kuepuka maumivu.

Kwa mfano, kama una shilingi milioni moja, ukaambiwa ipo fursa ya kutumia milioni hiyo moja kupata milioni nyingine, lakini pia unaweza ukapoteza hiyo milioni moja uliyonayo, wengi husita kuchukua hatua.

Na kwa hakika, hii ndiyo inawazuia watu wengi kuchukua hatua. Tunaogopa sana kupoteza kuliko kuhamasika kupata. Tupo tayari kulinda kile tulichonacho, hata kama ni kidogo kuliko kuchukua hatua na kupata kikubwa zaidi.

Na hii ndiyo sababu watu wengi wanaendelea kubaki kwenye ajira ambazo kipato hakiwatoshelezi, lakini wanahofia kupoteza hata hicho kidogo.

Jua

Wengine wanaendelea kubaki kwenye biashara zile zile, ambazo hazikui wala kupiga hatua, hawabadili na kupiga hatua zaidi kwa sababu wanaogopa kupoteza kile kidogo walichonacho.

Kuondokana na hofu hii, unapaswa kubadili fikra zako juu ya kile ulichonacho. Acha kukiona kama usalama na badala yake ona kama kikwazo cha wewe kupiga hatua zaidi.

Wanasema adui wa ubora ni uzuri, watu wengi wakishapata kitu kizuri wanaridhika na kujisahau, na hilo huwazuia kupata kilicho bora zaidi.

Hivyo mara zote kuwa tayari kuchukua hatua ya kuboresha zaidi ile hali uliyonayo. Chukua hatua hata kama ni ndogo, lakini iwe ya kuboresha zaidi pale ulipo.

SOMA; UKURASA WA 398; Nitaanza vizuri wiki ijayo…

Usihofie sana kupoteza, kwa sababu kuendelea kubaki hapo bila ya kuchukua hatua, unapoteza mengi zaidi ya hayo unayolinda sasa.

Na hata kama utapoteza kile unachohofia kupoteza, kumbuka utajifunza mengi pia, hivyo utakuwa bora zaidi ya ulivyokuwa kabla hujachukua hatua.

Hatua yoyote unayochukua, hata kama utashindwa, hutabaki pale ulipo, badala yake utajifunza mengi zaidi. Na huo ni ushindi.

Tuache kukumbatia kile tulichonacho na kuogopa kuchukua hatua. Badala yake tuhamasike na kile kinachoweza kuwa bora, tuchukue hatua na kujifunza zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.