UKURASA WA 1019; Kama Huwezi Kuona Ubaya, Huwezi Kuona Uzuri Pia…

By | October 15, 2017

Mambo yamegawanyika katika makundi mawili, kuna mambo mazuri na mambo mabaya. Iwe ni watu, tabia, matokeo, juhudi ambazo tunaweka, kila kitu kinaweza kuwa kizuri au kibaya.

Sasa katika uzuri na ubaya, hakuna katikati, ni labda kitu ni kizuri, au kitu ni kibaya, kuwa katikati ni kutokuona uzuri wala ubaya.

Kama huwezi kuona ubaya kwenye tabia zako fulani ambazo zinakurudisha nyuma, hutaweza kuona uzuri kwenye kuachana na tabia hizo ili uweze kufanikiwa. Hivyo utaendelea na tabia hizo kwa sababu hakuna tofauti yoyote.

Kama huwezi kuona ubaya kwa baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa wanakurudisha nyuma, hutaweza kuona uzuri kwa watu ambao unaweza kushirikiana nao kusonga mbele. Hivyo hutaweza kunufaika kupitia wengine, kwa sababu utaona hakuna tofauti yoyote.

Kama huwezi kuona ubaya, hutaweza pia kuona uzuri, utaona mambo yote yapo sawa, na hapo utakosa fursa nzuri zinazopatikana kwenye uzuri.

Wakati mwingine watu wanaona ubaya, lakini wanajifanya hawajauona au wanakataa siyo ubaya. Labda kwa sababu ni kitu wanapenda kufanya na hivyo kuona ni kizuri, au ni watu wanaowapenda na hivyo kuona hawawezi kuwa wabaya.

SOMA; UKURASA WA 233; Ni Vikwazo Gani Unaendelea Kujiwekea Kwenye Maisha Yako.

Hivyo kama utakataa ubaya siyo ubaya, basi utakuwa uzuri kwako, na hilo litakuharibia zaidi. Kwa sababu utakumbatia ubaya kama uzuri, na kuukosa uzuri ambao upo wazi kabisa.

Utang’ang’ana na tabia mbaya zinazokurudisha nyuma, wakati zipo tabia nzuri nyingi tu. Utang’ang’ana na watu ambao wanakurudisha nyuma, wakati wapo watu wengi ambao wangekusukuma kwenda mbele.

Ni mpaka ukubali ubaya wa vitu fulani, ndipo utaweza kuona uzuri wa kukuwezesha kupiga hatua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.