UWEKEZAJI LEO; Maana Ya Gawio Katika Uwekezaji Na Utolewaji Wake.

By | October 19, 2017

Kampuni au taasisi ambayo inauza hisa zake kwenye soko la hisa, inapaswa kutoa hesabu zake za mwaka kila mwaka. Katika hesabu hizi kampuni itaonesha mapato, matumizi, faida na hata hasara.

Iwapo kampuni imepata faida mwisho wa mwaka wa fedha, faida ile inapaswa kurudi kwa wanahisa wa kampuni hiyo.

Ile sehemu ya faida ya kampuni inayolipwa kwa wanahisa ndiyo inaitwa gawio. Hichi ni kipato ambacho mwekezaji anapata kutokana na uwekezaji ambao amefanya.

Kupata gawio, hakupunguzi chochote kwenye hisa za mwekezaji, badala yake anakuwa amepata faida, huku hisa zake zikiendelea kuwa kama zilivyokuwa. Hivyo hata kama atapokea gawio kila mwaka kwa miaka mitano, akija kuamua kuuza hisa zake atapata thamani ya zile hisa.

Moja ya vigezo ambavyo wawekezaji hasa kwenye hisa wanashauriwa sana kuangalia ni utoaji wa gawio. Unaponunua hisa kwenye kampuni inayotoa gawio, unanufaika zaidi na uwekezaji wako.

Makampuni yanatofautiana kwa namna yanavyotoa faida yake kwa wawekezaji wake.

Zipo kampuni ambazo zinatoa gawio moja kwa moja, hapo zinatoa sehemu ya faida kwa wanahisa. Kiasi cha gawio hupatikana kwa kugawa faida inayotolewa kwa wanahisa kwa idadi ya hisa. Na hapo kinapatikana kiasi cha fedha kitakacholipwa kwa kila hisa moja.

Zipo kampuni ambazo faida inayopatikana inarudishwa kuwekezwa kwenye kampuni, ili kuikuza zaidi na kuongeza thamani ya hisa zake. Hapa wanahisa wananufaika kwa ongezeko la thamani kwenye uwekezaji wao.

Pia zipo kampuni ambazo zinaweza kutumia faida yake kununua hisa zake yenyewe, kutoka kwa wanahisa. Kama itanunua kwa bei nzuri wanahisa wananufaika.

SOMA; UWEKEZAJI LEO; Vodacom Wametangaza Kutoa Gawio La Kwanza Kwa Wawekezaji.

Utoaji wa gawio ni lazima uridhiwe na wanahisa kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa kampuni. Na ikisharidhiwa basi kila mwanahisa, kulingana na daraja la hisa zake anapata kile anachostahili, kwa idadi ya hisa anazomiliki.

Gawio ni faida ya moja kwa moja ambayo mwekezaji anaweza kuipata kutokana na uwekezaji wako. Hivyo unapochagua kampuni za kuwekeza kwa kununua hisa zake, kigezo cha utoaji wa gawio ni muhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

2 thoughts on “UWEKEZAJI LEO; Maana Ya Gawio Katika Uwekezaji Na Utolewaji Wake.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.