UKURASA WA 1023; Tatizo Siyo Waliokuzunguka, Tatizo Ni Wewe…

By | October 19, 2017

Wapo watu wengi ambao wamekwama, wameshindwa kupiga hatua walizopanga kupiga. Ukiwauliza kwa nini wameshindwa, au pale wanapojiuliza wao wenyewe, wanasema wale waliowazunguka ni kikwazo kikubwa kwao kupiga hatua.

Labda ni mwajiriwa ambaye mwajiri wake amekuwa kikwazo, au wafanyakazi wenzake wamekuwa changamoto kwake.

Au ni mtu ambaye mwenza wake amekuwa kikwazo na changamoto kwa mafanikio yake.

Yawezekana pia ni marafiki wa karibu, ambao wanakuwa wanamfanya mtu ashindwe kuchukua hatua na kufanikiwa.

Ni kweli wale wanaotuzunguka, kuna hatua wanaweza kuchukua au kushindwa kuchukua na hiyo ikapelekea sisi kukwama kwenye mipango tuliyokuwa nayo.

Lakini hiyo haipaswi kuwa sababu ya kumzuia mtu kufanikiwa. Hupaswi hata dakika moja kukaa na kulaumu kwamba wanaokuzunguka wamekukwamisha.

Badala yake unahitaji kuchukua hatua.

Kwa sababu, kumbuka wewe siyo mti, kwamba lazima uwe hapo ulipo wakati wote. Unao uwezo mkubwa wa kubadili chochote ambacho kinakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.

Hivyo chochote ambacho unaona kinakuzuia wewe kufanikiwa, kibadili, kibadili mara moja kama inawezekana, na kama haiwezekani kibadili taratibu, kama hakibadiliki basi badilika wewe.

SOMA; UKURASA WA 903; Njia Bora Ya Kuwapima Wanaokuzunguka Kama Wanakufaa…

Muhimu zaidi kama kuna mtu anapaswa kulaumiwa kuhusu wanaokuzunguka, basi ni wewe mwenyewe, ndiyo namaanisha wewe.

Kwa sababu, wewe ndiyo umewavutia hao wanaokuzunguka, kwa namna unavyofanya mambo yako na kwa vitu unavyovumilia, ndiyo unawakaribisha wengine waone wewe ni wa aina yao.

Hivyo ukitaka kuwakimbiza wale ambao hawakufai, huhitaji haya kugombana nao. Bali unahitaji kuishi misingi yako ya maisha ya mafanikio, na usikubali kuipindisha kwa namna yoyote ile. Wale wanaoiweza misingi hiyo wataendelea kuwa na wewe, na wale wasioiweza hawataweza kuwa na wewe.

Usiendelee tena kusema tatizo ni wanaokuzunguka, tatizo ni wewe, hivyo chukua hatua sasa ili uweze kuondokana na wale wanaokurudisha nyuma na uweze kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.