Barua ya XV; Kujenga afya ya akili na roho.

By | August 11, 2023

Barua ya XV; Kujenga afya ya akili na roho.

Rafiki yangu Mstoa,
Sisi binadamu tuna mwili, akili, roho na hisia.
Lakini inapokuja kwenye kujenga afya zetu, huwa tunahangaika zaidi na afya ya mwili na kusahau hizo afya nyingine.
Angalia gharama ambazo watu huwa wanaingia kwenye kujenga afya ya mwili, kuanzia ulaji, mazoezi na hata mavazi.
Ni gharama kubwa sana ambazo watu hutumia kwenye mwili, huku wakisahau akili, roho na hisia.

Tunaweza kudhani hili limeanza zama hizi ambapo anasa zimekuwa nyingi.
Lakini ni jambo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu.
Inaonekana ni tabia yetu binadamu kuhangaika zaidi na kile tunachoona na kupuuza tusichoona.
Ndiyo maana tuhangaika zaidi na miili yetu ambayo tunaiona na kupuuza akili, roho na hisia ambazo hatuzioni.

Mwanafalsafa wa Ustoa Seneca aliliona hilo na kumwandikia rafiki yake Lucilius kwenye barua yake ya 15.
Karibu tujifunze kwenye barua hii jinsi ya kujenga afya ya akili na roho ili tuweze kujenga maisha bora na ya mafanikio.

1. Afya ya akili inajengwa kwa falsafa.

Seneca anaanza kwa kueleza kwamba afya ya akili huwa inajengwa kwa falsafa.
Na afya ya akili ndiyo kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza cha kila mtu, kwani ndiyo inaongoza hata afya ya mwili.
Kama afya ya akili haitakuwa sawa, afya ya mwili pia haitaweza kuwa sawa.

Seneca anaendelea kueleza kwamba ni upumbavu kuweka juhudi kubwa kujenga afya ya mwili, kwa kuwa na misuli imara na mabega mapana huku ukisahau afya ya akili.
Kwa sababu hata uwe na mwili imara kiasi gani, huwezi kumshinda nguvu ng’ombe dume.

Hapo Seneca anamaanisha uimara wetu sisi binadamu haupo kwenye mwili, bali kwenye akili, roho na hisia.
Kwa kujenga akili imara, hivyo vingine vyote vitaweza kuwa vizuri.

Hatua ya kuchukua;
Weka kipaumbele cha kwanza kwenye kujenga afya yako ya akili kupitia falsafa ya Ustoa. Jifunze na kuiishi misingi ya Ustoa na utaweza kujenga utulivu mkubwa kwenye maisha yako.

Nukuu;
“Without philosophy the mind is sickly, and the body, too, though it may be very powerful, is strong only as that of a madman or a lunatic is strong.” – Seneca

“Bila ya falsafa akili inakuwa na ugonjwa, na mwili pia unakuwa na ugonjwa, japo unaweza kuonekana imara, hautofautiani na wa mwendawazimu.” – Seneca

2. Kula na kufanya mazoezi ya mwili.

Seneca anaeleza jinsi ambavyo huwa anashangazwa na watu wanavyoendesha maisha yao.
Kwanza wanakula chakula kingi kupitiliza, kitu ambacho kinachosha mwili, akili na roho.
Chakula hicho wanachokula kwa wingi kinapelekea wawe na uzito uliopitiliza.
Na hivyo wanalazimika kufanya mazoezi ili kupunguza uzito wanaokuwa nao.

Seneca anaeleza mfumo huo wa maisha ambao wengi ndiyo wanao una hasara nyingi sana.
Kwanza unashusha hadhi ya maisha ya mtu kwa jinsi afya yake inavyokuwa siyo sahihi.
Pili mtu anapoteza muda wake mwingi kwenye kula na kufanya mazoezi, kitu ambacho hakina tija kabisa, yaani unakula kwa wingi halafu unalazimika kufanya mazoezi ili kutumia chakula kingi ulichokula.
Tatu ni watu wanageuka kuwa watumwa wa miili yao, kwa kulazimika kuitimizia tamaa mbalimbali.

Seneca anashauri kuwa na udhibiti kwenye ulaji kwa kula kwa kiasi na pale tu inapobidi. Hatupaswi kula kwa sababu ni muda wa kula au chakula kipo.
Bali tunapaswa kula pale tunapokuwa na njaa na kula kwa kiasi, siyo mpaka kushiba kupitiliza.

Kwa upande wa mazoezi Seneca anashauri tufanye mazoezi ya muda mfupi ambayo yanahusisha viungo vyote vya mwili na yanauchosha mwili haraka. Mazoezi anayopendekeza ni kukimbia, kuruka na kunyanyua vitu vizito.
Tunapaswa kutumia muda mfupi sana kwenye mazoezi ya mwili ili kupeleka muda mwingi kwenye vitu muhimu zaidi, kama kujenga akili ya mwili.

Hatua ya kuchukua;
Kula mara chache kwa siku, mara moja au mbili na kula kwa kiasi, siyo mpaka ushibe kabisa.
Fanya mazoezi yanayochosha mwili haraka na kwa muda mfupi.

Nukuu;
“Now there are short and simple exercises which tire the body rapidly, and so save our time; and time is something of which we ought to keep strict account.” – Seneca

“Kuna mazoezi rahisi na mafupi yanayouchosha mwili haraka na kuokoa muda; na muda ndiyo kitu tunachotakiwa kukilinda sana.” – Seneca.

3. Mazoezi ya akili.

Seneca anasema akili inatakiwa kufanyiwa mazoezi usiku na mchana. Kwa sababu akili inalishwa kwa kazi ambazo inapewa kwa kiasi.
Mazoezi ya akili yanapaswa kufanywa kwa msimamo mara zote bila kuathiriwa na hali ya hewa au mambo mengine yoyote.
Anasisitiza mazoezi ya akili hayapaswi kuathiriwa na hali ya uzee. Kwani akili inapaswa kuwa imara kadiri mtu anavyozidi kuzeeka.
Kujenga afya ya akili kunaifanya akili kuwa bora kadiri mtu anavyozeeka.

Lakini Seneca anatutahadharisha kwamba kuipa akili mazoezi haimaanishi muda wote mtu kuwa unasoma au kuandika. Hayo ni muhimu kuyafanya kila siku. Lakini zipo njia nyingine za kuipa akili mazoezi, kama kufanya matembezi huku ukitafakari kwa kina.
Muhimu ni kuhakikisha huiachi akili yako ikazurura tu, badala yake unaielekeza kwenye kitu ulichochagua.
Hivyo ndivyo unavyoifanya akili yako kuwa imara mara zote.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku tenga muda wa kusoma, kuandika na kutafakari na tekeleza hayo bila kuruhusu kitu chochote kuingilia.
Usiache akili yako ikazurura tu, bali ielekeze kwenye kitu fulani. Hata kama umepumzika, elekeza akili yako kwenye kitu unachochagua wewe ili uendelee kuwa na udhibiti nayo.

Nukuu;
“The mind must be exercised both day and night, for it is nourished by moderate labour; and this form of exercise need not be hampered by cold or hot weather, or even by old age. Cultivate that good which improves with the years.” – Seneca

“Akili inapaswa kupewa mazoezi usiku na mchana, kwa sababu inalishwa kwa kupewa kazi kwa kiasi; mazoezi ya akili hayapaswi kuzuiwa na hali ya hewa au umri wa uzee. Tengeneza kilicho kizuri ambacho kinaendelea kuwa bora kadiri miaka inavyokwenda.” – Seneca

4. Kushukuru kunajenga afya ya roho.

Seneca anatushirikisha zoezi bora la kujenga afya ya roho ambalo ni kushukuru.
Kuwa mtu wa shukrani kunakujengea hali ya kuridhika na kuthamini kile ambacho tayari unacho.
Kwa sababu maisha ya wengi yamekuwa yanatawaliwa na tamaa ambayo haitoshelezeki.
Kila hatua ambayo mtu anapiga ndiyo anakuwa na tamaa ya kupiga hatua kubwa zaidi.
Tamaa ni adui mkubwa kwenye afya ya roho. Na tiba ya tamaa ni kuwa na shukrani.
Unaposhukuru unakuwa umethamini kile ambacho umeshakipata na hivyo kuona maisha yako yameshakamilika.
Tamaa inafanya mtu uone maisha yako hayajakamilika mpaka upate kile unachotamani.
Na hata ukikipata, siyo ndiyo unaridhika, badala yake tamaa inakuwa kubwa zaidi.

Seneca anasisitiza kwamba tamaa haiwezi kutibiwa kwa kuitimiza, bali inazidishwa zaidi.
Anasema kama kungekuwa na kitu kimoja ambacho tukishakipata basi tamaa yetu inaisha, tayari tungeshafikia hicho huko nyuma. Kwa sababu tayari tumeshapata vitu vingi sana tulivyovitamani, ila bado tamaa haijaondoka.
Ndiyo maana anasisitiza tuwe watu wa shukrani kama tiba pekee ya tamaa.
Tufanye zoezi la kushukuru ili kujiimarisha kiroho na kuondokana na msukumo wa tamaa.

Hatua ya kuchukua;
Shukuru kwa kila jambo kwenye maisha yako. Kila siku tenga muda wa kufanya zoezi la shukrani. Unafanya zoezi hilo kwa kuchukua kalamu na karatasi na kuandika vitu vitano unavyoshukuru kuwa navyo kwenye maisha yako.
Zoezi hilo linakupa utulivu mkubwa wa kiroho.

Nukuu;
“The fool’s life is empty of gratitude and full of fears; its course lies wholly toward the future.” – Epicurus

“Maisha ya mpumbavu yana utupu wa shukrani na yamejawa na hofu; mwenendo wake wote umeegemea siku zijazo.” – Seneca

“For we are plunged by our blind desires into ventures which will harm us, but certainly will never satisfy us; for if we could be satisfied with anything, we should have been satisfied long ago.” – Seneca

“Tunasukumwa na tamaa zetu kwenye mambo ambayo ni hatari kwetu, na bado hayawezi kuturidhisha; kwa sababu kama tungekuwa wa kuridhika, tayari tungesharidhika muda mrefu uliopita.” – Seneca

5. Jiwekee ukomo wa tamaa.

Tumeona jinsi ambavyo tamaa haziridhiki na hilo kutudhoofisha kiroho.
Lakini pia hatuwezi kuendesha maisha yetu bila ya tamaa kabisa.
Tamaa ndiyo zinatusukuma kuwa na maisha bora.
Tamaa zinakusa mbaya pale zinapotutawala na kutunyima furaha.
Na hilo hutokana na kukosa ukomo wa tamaa. Kila wakati tamaa zetu kukua zaidi pale tunapozifikia.

Seneca anatuambia njia bora ya kudhibiti tamaa ni kuweka ukomo ambao hutauvuka. Kwa kuwa na ukomo huo, utaweza kufurahia kila ulichonacho.
Unaya wa tamaa isiyo na ukomo ni kila unapoifikia, unapata tamaa ya makubwa zaidi ya ambayo umeshapata.
Hilo linakuzuia usiweze kufurahia kile ambacho umeshakipata.

Seneca anasema kila kitu kwenye maisha huwa kinaonekana ni kizuri kabla mtu hajakipata. Lakini akishakipata anakiona ni cha kawaida na kutaka kupata kingine kikubwa zaidi.
Na hata hicho kingine kikubwa mtu anachotaka, hakina chochote ambacho kitamrishisha.
Maana kama mtu angekuwa ni wa kuridhishwa na vitu anavyopata, angesharidhika muda mrefu huko nyuma, maana ameshapata vingi sana alivyokuwa anatamani kuvipata.

Seneca anasisitiza tusiyaharibu maisha yetu kwa tamaa zisizo na ukomo, hasa kutegemea vitu ambavyo bado hatujavipata.
Badala yake tuweke ukomo kwenye tamaa zetu na kufurahia yale ambayo tayari tumeshayapata.

Hatua ya kuchukua;
Jiwekee malengo ambayo utayafanyia kazi kuyafikia. Lakini ridhika na yale ambayo tayari umeshayapata. Furaha yako isisubiri kuyafikia malengo, bali furaha yako inapaswa kutokana na hatua unazopiga kuyaendea malengo yako.

Nukuu;
“They look better to those who hope for them than to those who have attained them.” – Seneca

“Vitu huwa vinaonekana ni bora kwa wale wanaovitumainia kuliko wale ambao tayari wameshavipata.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, kama umekuwa unakazana kujenga afya ya mwili na kusahau ya akili na roho, umekuwa unajipunja na ndiyo maana maisha yanakosa utulivu.
Anza sasa kujenga afya ya akili na roho kila siku kwa kufanya mazoezi tuliyojifunza hapa.
Kwenye afya ya akili tenga muda wa kusoma, kuandika na kutafakari kila siku.
Na kwenye afya ya roho, kila siku tenga muda wa kuandika vitu vitano unavyoshukuru kuwa navyo kwenye maisha yako.

Ukifanya mazoezi hayo kila siku kwa msimamo bila kuacha utaona maisha yako yakizidi kuwa bora huku ukiwa na utulivu mkubwa.
Lakini pia utaweza kujenga mafanikio makubwa na ambayo unayafurahia na kuridhika nayo.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.

Category: FALSAFA YA USTOA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

6 thoughts on “Barua ya XV; Kujenga afya ya akili na roho.

 1. Alex Kamata#MchinaWaMwanza

  Kwenye afya ya akili tenga muda wa kusoma, kuandika na kutafakari kila siku.
  Na kwenye afya ya roho, kila siku tenga muda wa kuandika vitu vitano unavyoshukuru kuwa navyo kwenye maisha yako.

  1.Nashukuru kuweza kuishinda hofu.
  2.Nashukuruku kuwa mwanafunzi ninayependa kujifunza katika haya maisha .
  3.Nashukuru kuweza kujua maisha yangu ni jukumu langu kwa asilimia 100, sina malalamiko kwa yeyote
  4.Nashukuru kwa ridhiki hii inayopatikana.
  5.Nashukuru kwa kuzikabili changamoto mbalimbali ninazokukana nazo .

 2. nderahisho

  Hili la shukran nilikuwa nafanya siku za nyuma nikaacha. Nitaendelea kuwa mtu wa Shukran sana kwani nina mengi sana sana ya kushukuru mpaka sasa.

 3. Miraji Luwi

  Asante Sana kocha
  Nimefurahi Sana na kupata msukumo hasa nilipsoma kwamba jinsi unavyokuwa na umli mkubwa ndivyo unavyopaswa kuwa na maaliza zaidi kupitia kuipa mazoezi akili.
  Ninaahidi kuyazingatia yote niliyojifunza toka ktk hii
  BALUA ya tisa. Asante kocha

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.