UKURASA WA 731; Sababu Moja Ya Kukufanya Uingie Au Uendelee Kubaki Kwenye Biashara Yako…

By | December 31, 2016

Tunaishi kwenye kipindi ambacho kuna fursa nyingi za kibiashara kuliko wakati mwingine wowote. Mtu aliyeishi miaka 200 iliyopita, akipata nafasi ya kurudi duniani leo, atashangazwa sana na fursa hizi zilizopo sasa.

Zamani ilikuwa kuingia kwenye biashara siyo kitu rahisi, mazingira yalikuwa magumu, ushindani mkali na masoko madogo. Lakini sasa hivi mazingira yamekuwa rahisi, ushindani upo lakini masoko yametanuka. Sasa hivi unaweza kuuza kitu popote pale bila hata ya kuwa na eneo rasmi la biashara.

SOMA; Kitu Pekee Kitakachokuletea Utajiri Kwenye Maisha Yako Ni Hiki…

Lakini pia kwenye wakati huu wa fursa nyingi za kibiashara, ndiyo wakati ambao watu wengi sana wamepotezwa na fursa hizi. Umekuwa ni wakati ambao watu wanafukuzana na fursa lakini wasiweze kunufaika na fursa hizo. Watu wanashawishika biashara fulani ni nzuri, wanaikimbilia na wakishafika ndani wanagundua mambo siyo rahisi kama walivyofikiri awali.

Leo nataka nikupe sababu moja ya msingi ya kukufanya uingie kwenye biashara, au kama tayari upo kwenye biashara basi itakayokufanya ubaki kwenye biashara hiyo. Kama sababu hii hutakuwa nayo, usiingie kwenye biashara, na kama tayari upo kwenye biashara basi jipange kufanya mabadiliko.

Sababu yenyewe ni wewe kuamini kwenye ile biashara unayokwenda kuingia au unayofanya. Kuamini kwamba kipo kitu ambacho watu wanakipata kupitia biashara hiyo. Kuwa tayari kuweka juhudi kubwa kuhakikisha kwamba biashara hiyo inakuwa na mchango mkubwa kwa wengine, inaongeza thamani kwenye maisha ya wengine.

SOMA; Sababu Halisi Ya Watu Kukuambia

Kinyume na hapo, hufiki mbali. Haijalishi faida unapata kubwa kiasi gani, au ni fursa maarufu kiasi gani, mwisho wa siku vumbi litatua, moshi utapita na watu watauona ukweli.

Bilionea mwekezaji Warren Buffet ana kauli yake kwamba mawimbi yakitulia ndiyo utaona wazi nani anaogelea akiwa uchi. Akiwa na maana kwamba wakati wa habari za moto moto za fursa kila mtu anaweza kuingia, lile wimbi la fursa linapopita, ndiyo tunaona nani alikuwa kwenye biashara kweli na nani alichukuliwa tu na wimbi la fursa.

Rafiki, usiogelee uchi, hata kama mawimbi ni makubwa, kumbuka baada ya muda mawimbi yatatulia. Jua na amini kwenye chochote unachofanya, usichukuliwe na mawimbi ha habari za motomoto.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.