UKURASA WA 728; Sababu Halisi Ya Watu Kukuambia HAPANA…

By | December 28, 2016

Kama kuna neno utakalolisikia mara nyingi pale unapochagua maisha ya mafanikio basi ni HAPANA.

Kuna mambo mengi ambayo utakuwa unataka kufanya lakini wengine wanakuambia hapana. Kuna biashara nzuri utakazokuwa umeanzisha lakini wale ambao utakuwa umewafikiria kuwa wateja wako watakuambia hapana.

Unaweza kuwa na wazo zuri ambalo unahitaji watu wakuunge mkono, una hamasa kubwa juu ya wazo hilo, lakini wale ambao ungetegemea wakuunge mkono wanakuambia HAPANA.

Sasa tatizo kubwa siyo kwenye neno HAPANA, bali tatizo kubwa lipo kwenye namna watu wanavyolichukulia neno hapana. Watu wengi wamekuwa wakiogopa sana neno hapana, hivyo wanaingiwa na hofu na hivyo kushindwa kabisa kuchukua hatua.

Kwa kuwa watu wanahofia kuambiwa hapana, basi hawaulizi kabisa, au hawatoi mapendekezo yao kabisa. Hii imekuwa inatokana na watu kuona kwamba wanapoambiwa HAPANA basi wao hawafai. Unapomwambia mtu kitu ambacho wewe unakiamini, umekifanyia kazi na una hamasa kubwa, halafu akakuambia hapana, unavunjika moyo sana. Hii inakufanya uanze kujihoji kama kweli unachotaka kina maana au unapoteza tu muda wako. Unapokutana na hapana hizi mara kadhaa, unaamua kuacha na kukubali kwamba waliokuambia hapana wapo sahihi.

Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba wanaokuambia hapana wapo sahihi, ila siyo kwa namna unavyochukulia wewe. Wanaokuambia hapana wapo sahihi kwa upande wao, labda hawataki hicho unachotaka kuwapa, au hawana taarifa za kutosha au basi tu hawajavutiwa. Hii ina maana kwamba wanakuambia hapana kwa sababu zao binafsi, na siyo kwa sababu yako.

Hivyo ina maana watu wakikuambia hapana, wamesema hapana kwa kile ulichowaambia na siyo hapana kwako wewe. Yaani watu hawakukatai wewe, bali wanakataa kile unachowaambia au unachowataka wafanye. Kwa maana hiyo hakuna haja ya wewe kukata tamaa pale watu wanapokuambia hapana. Hakuna haja ya kujiona hufai na kuacha, badala yake jua hujawapata watu sahihi bado na hivyo endelea kuuliza wengine wengi zaidi.

Ninachotaka utoke nacho hapa rafiki ni kwamba kuambiwa hapana kusiwe mwisho wa wewe kuuliza au kuuza au kutoa mapendekezo yako. Usihofie kuchukua hatua kwa sababu watu wanasema hapana. Badala yake endelea na utakutana na watu sahihi, ambao kwa kukusikia tu watasema NDIYO na mambo yako yatakwenda vizuri.

Zoea neno HAPANA, utakutana nalo mara nyingi sana kwenye maisha yako hapa duniani. Usikubali liwe kikwazo kwako, endelea kusonga mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 728; Sababu Halisi Ya Watu Kukuambia HAPANA…

  1. Pingback: UKURASA WA 731; Sababu Moja Ya Kukufanya Uingie Au Uendelee Kubaki Kwenye Biashara Yako… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.