Watu wana matatizo yao, na wewe una matatizo yako, unachopaswa kuelewa vizuri kabisa ni kwamba matatizo ya watu siyo matatizo yako.
SOMA; Watu Wana Matatizo Yao, Hawataki Kusikia Yako….
Na hapa tunakwenda kuzungumzia kwenye upande wa kazi na biashara.
Kumekuwa na mazoea ya mfanyabiashara au mtoa huduma kutumia matatizo yake kama sababu ya kushindwa kutatua matatizo ya mteja wake. Labda mteja hajapata huduma nzuri na wewe unamweleza kwamba na wewe pia una matatizo fulani au unampa changamoto zako ambazo zimekupelekea wewe kushindwa kumpa huduma anayohitaji.
Mteja anaweza kukusikiliza, lakini kumbuka kilichomleta kwako siyo matatizo yako, bali ni matatizo yake. Hivyo kama wewe hutaweza kumtatulia matatizo yake basi atatafuta yanapoweza kutatuliwa na akipapata, hutamwona tena mteja huyo.
Ni lazima uelewe kwamba kazi au biashara yoyote unayofanya, upo pale kuwasaidia watu kuondokana na matatizo yao, au kuwapatia mahitaji yao. Hicho ndiyo watu wanachotegemea wanapofika kwenye eneo lako.
Sasa wanapofika na badala ya kupata kile wanachofuata wanajikuta wanabeba matatizo yako, hawawezi kuvumilia hilo, na kwa kuwa wanaofanya kama unachofanya wewe ni wengi, basi watatafuta sehemu nyingine ya kupata huduma wanazohitaji.
Usimlalamikie mteja namna unavyopata changamoto kwenye biashara yako na kutumia hiyo kama sababu.
Usitafute sababu za kuhalalisha kushindwa kwako kumpa mteja huduma aliyotegemea kupata.
Weka matatizo yako pembeni, weka changamoto zako pembeni na ule muda mchache unaoupata na mteja wako, hakikisha unamhudumia kwa ubora kabisa, hakikisha anaondoka akiwa ameridhika na kesho atakuja tena, yeye na wengine zaidi.
Kumbuka kila unapotaka kuyatumia matatizo yako kama sababu kwamba matatizo yako wewe siyo matatizo ya mteja wako. Tatua kwanza matatizo yake au tatua kwanza yako ndiyo uendelee na kazi au biashara yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK