UKURASA WA 774; Anza Kuamini Ukweli Huu….

By | February 12, 2017

Jambo moja ambalo halipingiki ni kwamba safari yako ya mafanikio itakuwa ngumu, yenye changamoto na vikwazo vingi kuliko ulivyokuwa ukidhani wakati wa kuanza. Watu uliotegemea wangekuwa msaada kwako inakuwa tofauti. Uliotegemea wangekuwa nyuma yako kukupa moyo, wanakuwa wa kwanza kukukatisha tamaa, kukucheka na hata kukubeza.

Lakini hayo ni madogo, makubwa zaidi yanakuja pale ambapo kitu ulichokuwa unaamini unakiweza, ulichokuwa huna shaka kabisa kwamba unaweza kushindwa, unashindwa. Unaanza kwa matumaini makubwa, ukiwa na hamasa kwamba unaweza kufanya makubwa, ila mwanzo kabisa unashindwa, unaanguka na kutokufikia pale ulipopanga kufika.

Hatua hii ndiyo inayoua ndoto za wengi, ndiyo inayowafanya wengi kuamua kuacha safari ya mafanikio na kurudi kwenye maisha ya kawaida. Ndiyo inawafanya watu waamini wale waliokuwa wanawakatisha tamaa walikuwa sahihi.

Lakini wewe rafiki yangu, wewe uliyechagua kuwa mwanamafanikio sikuruhusu kabisa ufanye hivyo. Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba UNAHITAJI KUAMINI UKWELI, na ukweli ni kwamba hata kama umeshindwa mara ngapi, bado uwezo wako ni mkubwa, bado wewe ni wa kipekee na bado unaweza kufanikiwa. Kushindwa mara moja, mbili hata mara mia moja, hakuondoi ukweli huu, ukweli unabaki kuwa ukweli mara zote, kinachobadilika ni muda tu wa kufikia kile unachotaka.

SOMA; Hatua Sita Za Kuuchuja Ukweli Na Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuukaribia Ukweli.

Nakukumbusha uamini katika ukweli, na kamwe usiamini kwenye maoni ya watu. Kila mtu anaweza kuwa na maoni yake juu yako, kama utafanikiwa au la, lakini ni wewe tu unayeweza kuujua ukweli uliopo ndani yako. Hakuna mwingine mwenye nafasi hii. Amini ukweli ulio ndani yako na acha kuyumbishwa na maono ya wengine.

Kushindwa siyo mwisho wa safari mpaka wewe mwenyewe kwa ridhaa yako utakapochagua iwe mwisho wa safari. Acha mapambano yaendelee, hakuna aliyekuahidi kwamba yatakuwa rahisi, lakini ukweli ni kwamba unaweza kupambana na chochote kitakachokuja mbele yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.