UKURASA WA 775; Mabadiliko Ya Haraka Yanashindwa Haraka…

By | February 13, 2017

Pale mtu anapopata ufahamu, anapotoka kwenye giza la kukosa maarifa, hupenda kufanya mabadiliko ya haraka sana.

Mtu anapojua kwamba alikuwa haweki akiba, na hivyo kuchagua kuweka akiba, hutaka kuweka akiba kubwa kwa kuanza.

Au pale mtu anapogundua kwamba alikuwa hafanyi mazoezi na mazoezi ni muhimu kwake, hupanga kuanza mazoezi makubwa na ya haraka.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa wale wanaotaka kuacha ulevi wowote ambao wamekuwa nao kwa muda mrefu. Kuacha ghafla na mara moja.

Chochote kile ambacho mtu anaona amechelewa kufanya, basi hushawishika kufanya kwa kiasi kikubwa na kufanya haraka zaidi.

SOMA; Wakati Sahihi Wa Kufanya Mabadiliko Ni Huu…

Lakini miili yetu ilishazoea hali ya mwanzo, hali ya kutoweka akiba, hali ya kutokufanya mazoezi, hali ya kutegemea ulevi. Hivyo unapokazana kuutoa mwili haraka kwenye hali ambayo umeshaizoea, mwili unakupinga na unahakikisha unarudi kwenye hali iliyozoeleka. Siyo kwa sababu mwili unashindana na wewe, bali kwa sababu mwili una kazi moja ya kulinda kile kilichozoeleka.

Hivyo unapotaka kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako, anza kidogo kidogo. Anza na hatua ambazo hazitaleta madhara makubwa ya wakati mmoja. Kama ni kuweka akiba anza na kiasi kidogo ambacho hakitaleta tofauti kubwa kwenye matumizi yako ya sasa. Kama ni mazoezi anza na hatua ndoto ambazo hazitauumiza mwili sana.

Ukianza na hatua kubwa kwa haraka, hutafika mbali, kwa sababu utakutana na kila sababu inayokuzuia wewe kuendelea na mabadiliko hayo. Mabadiliko yoyote unayopanga kufanya kwenye maisha yako, anza na hatua ndogo, anza na asilimia moja na fanya kila siku, huku ukiendelea kuongeza kiasi.

Unaweza kuanza kwa hatua kubwa kama kweli umechoshwa, ila jiandae kabisa na upinzani ambao mwili wako na mazingira yako yataleta kwenye mabadiliko hayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.