UKURASA WA 778; Nguvu Iliyopo Katika Kundi…

By | February 16, 2017

Moja ya maeneo ambayo nimewahi kuyaandikia sana, hasa linapokuja swala la mafanikio, ambalo ndiyo msingi wetu mkuu, ni kuepuka kundi. Tumeona namna ambavyo makundi yanawapoteza watu. Pale watu wanapofanya kitu kwa sababu kila mtu anafanya, hapo ndipo ndoto za wengi zinapopotea.

together-in-unity

Kundi kubwa la kijamii limepoteza watu wengi mno. Wapo watu ambao wanaamka kila siku asubuhi na mapema, kwenda kwenye kazi ambazo hawazipendi na pia haziwalipi vizuri, huku wakijua kabisa zipo fursa nyingine ambazo wangeweza kuzitumia lakini wanashindwa kuondoka kwenye kazi hiyo kwa sababu kila mtu anayemzunguka yupo kwenye kazi. Anaona ataonekanaje pale atakapoondoka kwenye kazi, kitu ambacho kila mtu anakijua kwake.

Kundi limepoteza wengi zaidi kwenye zama hizi za fursa za kibiashara. Wapo watu ambao wamekuwa wanaibuka na fursa za kibiashara ambazo siyo sahihi au ni za kitapeli, wanatafuta kundi la watu wenye  tamaa ya mafanikio, wanawashawishi kuingia kwenye fursa hiyo, na kundi linaendelea kuwavutia wenye tamaa zaidi, mwisho hata wasio na tamaa wanajikuta wameingia kwa sababu karibu kila mtu yupo kwenye fursa hiyo hivyo wengi wanafikiri kwa kuwa watu wengi wanakubaliana na fursa hii, basi itakuwa kweli.

Imekuwa inaelezwa kila mara ya kwamba hapo ulipo ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Ukiangalia maisha uliyonayo, mafanikio uliyonayo na hata namna unavyofanya mambo yako, hutofautiani sana na wale watu watano wa karibu sana kwako.

SOMA; Kama Hutaki Kubaki Kwenye Kundi….

Hakika kundi lina nguvu kubwa sana ya kubadili maisha yako, liwe kundi dogo au kubwa, ukishakuwa ndani ya kundi hilo, unabadilishwa.

Sasa leo nataka tuangalie namna ya kutumia nguvu hii ya kundi katika kufikia mafanikio makubwa.

Kwa kuwa tunajua kundi linaweza kutubadili, basi sisi wenyewe tunachagua kuingia kwenye kundi ambalo lina zile sifa muhimu kwetu. Tunaanza na wale watu watano wa karibu sana kwetu, wale watu watano ambao tunakuwa nao muda mrefu. Tunahitaji kuwachunguza na kuona ni wapi wanataka kwenda, ni juhudi kiasi gani wanaweka kwenye shughuli zao. Chagua wale ambao wanaendana na wewe, wale ambao wana ndoto kubwa kama ulizonazo wewe.

Baada ya watu hawa watano, chagua kundi la kijamii ambalo utakuwa ndani yake. Kundi hilo liwe makini, lenye watu makini na wanaoishi kwa misingi ya mafanikio. Ndani ya kundi kama hilo unapata hamasa ya kufanya zaidi kutokana na wengine wanavyofanya.

KISIMA CHA MAARIFA ni moja ya makundi unayopaswa kuyatumia vizuri katika kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Unaweza kuangalia makundi mengine kama hayo ambayo yanakusukuma kufanikiwa.

Kwa maana hiyo basi, ondoka kwenye kila kundi ambalo halikusukumi mbele zaidi, kama kundi halikupi hamasa ya kufanikiwa, achana nalo mara moja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.