UKURASA WA 779; Usichukue Ushauri Kwa Mtu Wa Aina Hii…

By | February 17, 2017

Moja ya vitu ambavyo vinatolewa bure kabisa, na vinatolewa na kila mtu ni ushauri. Kila mtu anafikiri ana ushauri mzuri ambao anaweza kutoa kwa wengine. Na hata watu ambao hawana uzoefu wala uelewa wa mambo, nao wanaweza kushauri kulingana na wanavyosikia kutoka kwa wengine. Yaani mtu anasikia mtu akishauri, na yeye anatoka hapo na kwenda kushauri, bila hata ya kujua yule aliyeshauri ana sifa gani ya kuweza kutoa ushauri anaotoa.

Nimekuwa naandika mara nyingi, hakuna kitu chenye gharama kubwa kama ushauri wa bure. Huwezi kuona gharama ya ushauri wa bure na unaotolewa na kila mtu mpaka pale utakapotumia ushauri huo na ukakuumiza.

Leo nataka tuangalie aina ya watu ambao hupaswi kabisa kuchukua ushauri kwao. Haijalishi ushauri wao ni mzuri kiasi gani, kama tu wana sifa hii moja ninayoenda kukupa, basi hustahili kwa namna yoyote ile kuchukua ushauri wao.

SOMA; Pamoja Na Ushauri Mzuri Utakaopewa, Bado Kitu Hiki Utafanya Wewe Mwenyewe.

Watu ambao hupaswi kuchukua ushauri kwao hasa wa namna gani ya kufanya mambo yako na kufanikiwa, ni watu ambao wameshakata tamaa na ndoto zao. Watu ambao walianza na ndoto kubwa, wakaanza kuzifanyia kazi, wakakutana na changamoto kubwa na kuishia kukata tamaa, hawana kikubwa cha kukushauri juu ya namna unavyoweza kufikia ndoto zao.

Kama ushauri wao ni mzuri wangeutumia kwanza wao kufikia ndoto zao, lakini kama wameshindwa kuutumia wao kwa nini wanataka kukupa wewe?

Kitu pekee unachoweza kujifunza kwa mtu aliyekata tamaa ni kutokukata tamaa, mengine achana nayo, maana yanaweza kukupelekea na wewe kukata tamaa.

Mtu aliyekata tamaa anapoanza kukushauri kipi ufanye ili ufanikiwe, na wewe ukamsikiliza na kufanyia kazi, unafuata njia ya kushindwa na kukata tamaa. Ushauri anaokupa wewe kama alishindwa kuutumia na akakata tamaa, usiuchukue. Na kama alijifunza baada ya kukata tamaa, autumie kwanza yeye kabla hajakupa wewe.

Watu waliokata tamaa siyo watu wazuri sana kwako kwenye kufikia ndoto zako, wajue na kuwaepuka haraka ili wasikuangushe kwenye shimo la kukata tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 779; Usichukue Ushauri Kwa Mtu Wa Aina Hii…

  1. Pingback: UKURASA WA 781; Kujilisha Upepo… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.