UKURASA WA 790; Kazi Yako/Yao Siyo Kukusanya Pesa….

By | February 28, 2017

Mafanikio ya biashara yoyote, yanaanzia kwenye ule msingi ambapo biashara hiyo imejengwa. Biashara ikijengwa kwenye misingi sahihi inakua na kuleta faida kubwa. Lakini biashara inapojengwa kwenye misingi isiyo sahihi, haiwezi kufika mbali.

IMG-20170217-WA0007

Msingi wa biashara unamwathiri kila anayehusika kwenye biashara hiyo. Mara nyingi watu huanza biashara kwa sababu wanataka kuanza, hawaandiki misingi yoyote, lakini kuna misingi wao wenyewe wanaiamini, na hii ndiyo inaishia kuwa misingi ya biashara hiyo. Na hata pale wanapoajiri watu wa kuwasaidia kwenye biashara hiyo, nao wanabeba misingi ile ile.

Moja ya misingi muhimu ya biashara ni kujua kwa nini mpo pale, ni nini hasa mnakifanya kwenye biashara husika. Wapo watu ambao wanaanzisha biashara wakifikiri kazi yao ni kukusanya fedha kutoka kwa wateja, na kuwapa kitu wanachotaka. Msingi huu unaanza na mwenye biashara na baadaye anapoajiri watu, huu ndiyo unakuwa utaratibu. Mteja anataka nini, anaambiwa bei yake, kama anataka atoe hela apewe kama hataki basi aondoke.

SOMA; Acha Kutafuta Pesa Ambazo Hutazipata, Tafuta Hiki Kimoja Na Usahau Matatizo Yako Ya Pesa.

Mara nyingi kinachowafanya watu kununua au kutokununua siyo bei, bali jinsi gani wanavyojisikia wanapokuwa kwenye biashara husika. Kumbuka binadamu wote ni viumbe wa hisia, hivyo mara nyingi hisia zinatutawala. Na maamuzi yoyote ya kununua, ni maamuzi ya hisia.

Ndiyo maana unaweza kuona watu wanakwenda kununua kitu cha ghali wakati wangeweza kukipata kwa bei rahisi. Watu wanakunywa soda ya tsh 3,000/= kwenye hoteli ambapo wangeweza kupata soda hiyo hiyo kwa tsh 500/= mtaani. Yote hayo yanatokana na ile hisia ambayo inaambatana na kile kitu ambacho mtu ananunua.

Hivyo basi, biashara yako ijenge kwenye misingi ya kuwaridhisha wateja, kwa mahitaji yao ya bidhaa au huduma na hisia pia. Usiwe tu pale kukusanya fedha na kutoa bidhaa au huduma, bali kuwa pale kuweka tabasamu kwenye uso wa mteja wako. Kumfanya mteja wako ajisikie vizuri kuwa kwenye biashara yako. Na huu ndiyo uwe msingi wa biashara, ambao utafuatwa na kila anayehusika kwenye biashara yako.

Kumbuka biashara za zama hizi zinaendeshwa kwa mahusiano, wateja wananunua pale wanapoona wanajaliwa, pale ambapo wanapata hisia kwamba anayewauzia ni rafiki yao na anajali kuhusu maslahi yao. Ila unapokuwa kwa ajili ya kupata faida tu, unawapoteza wateja wengi.

Msingi wa biashara yako uwe kuwapa wateja mahitaji yao ya msingi, pamoja na kujenga mahusiano mazuri, kuweka tabasamu kwenye nyuso za wateja wako. Huhitaji kufanya makubwa kutimiza hilo, unahitaji kujali kuhusu wateja wako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.