UKURASA WA 795; Mshahara Au Faida Pekee Haitakufikisha Kwenye Utajiri.

By | March 5, 2017

Watu wengi wanapenda utajiri, lakini njia sahihi ya kufikia utajiri huo hawaijui. Na kwa kuwa hili halifundishwi popote, wanaishia kujaribu jaribu kila njia, wanajikuta wakipoteza muda na kutokuuona utajiri wenyewe.

IMG-20170217-WA0004

Kwanza kabisa wapo wale ambao hata hawajui utajiri ni nini. Wengi wanafikiri kuwa na kipato kikubwa ni utajiri, au kupata faida kubwa ndiyo utajiri. Haijalishi unalipwa kiasi kikubwa kiasi gani, kama inabidi wewe uwepo moja kwa moja ndiyo utengeneze kipato hicho, bado wewe hujaufikia utajiri.

Yaani ninachosema ni kwamba, kama unafanya kazi, na mshahara wako labda ni milioni ishirini kwa mwezi, kama ndiyo kipato pekee unachotegemea, wewe bado ni masikini. Hii ni kwa sababu ukiacha kufanya kazi, basi kipato hicho kinakauka mara moja. Maisha yako yanaweza kubadilishwa haraka sana na chochote kinachotokea.

SOMA; Ujue Uwekezaji Kwenye Hatifungani (BONDS) Na Faida Zake.

Hivyo pia kwenye biashara, wengi wamekuwa wanafikiri biashara inawapa uhuru, hivyo wanakazana na kupata faida kubwa, na kuona maisha ndiyo haya. Lakini inapotokea shida na biashara ile kufa, wanarudi sifuri na kuanza tena, au wanapata msuko suko mkubwa sana.

Ninachotaka kukukumbusha leo rafiki ni kwamba, kipato cha moja kwa moja, kinachotegemea uwepo wako ndiyo ukizalishe, hakiwezi kukufanya tajiri hata siku moja. Ndiyo unaweza kuona kipato chako ni kikubwa wakati unakipata, lakini kinapokauka, ndiyo unagundua kwamba ulikuwa umejificha kwenye moshi.

Utajiri halisi unatokana na nini?

Kama tumekuwa pamoja kwa muda mrefu, utakuwa unajua mpaka sasa tunapoelekea nataka kukuambia ni nini.

Utajiri wa kweli unatokana na uwekezaji, pale ambapo pesa yako inakufanyia wewe kazi, hata kama haupo moja kwa moja kwenye kile ambacho fedha yako inafanya. Unahitaji kuwa na uwekezaji mwingi, ili uweze kufikia utajiri kwenye kipato chako, iwe ni mshahara au faida ya biashara.

Sisemi uache mshahara au faida, ila ninachosema, sehemu kubwa ya mshahara au faida yako, iende kwenye uwekezaji. Wekeza sana, huko ndipo unapotengeneza fedha isiyo ya mawazo. Kwa sababu uwekezaji hauozi, fedha yako inafanya kazi, hata kama wewe umelala. Ni kweli uwekezaji una hatari ya kupoteza fedha, lakini kadiri unavyowekeza maeneo mengi na mbalimbali, unakuwa na uhakika zaidi.

Kwa kumalizia, wengi wamekuwa wanafikiri ukishakuwa na biashara huhitaji kuwa tena na uwekezaji, hiyo ni dhana potofu. Hata kama una biashara 10, unahitaji kuwa na uwekezaji ambapo fedha yako inakufanyia wewe kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 795; Mshahara Au Faida Pekee Haitakufikisha Kwenye Utajiri.

  1. Pingback: UKURASA WA 798; Njia Mbili Za Kuongeza Faida Na Moja Ya Kuepuka Sana…. – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.