UKURASA WA 801; Siku 800 Za Kuandika….

By | March 11, 2017

Katika makala hizi za kurasa, ambazo ni makala ninazoandika kila siku, yaani namaanisha kila siku, bila ya kuruhusu sababu yoyote iingilie kwenye uandishi wangu, nimeshavuka kurasa 800 za kuandika.

Kama ningesema lengo langu ni kuandika kurasa 800 au hata 1000, huenda lingeniumiza sana, kwamba sasa hizi kurasa zitaishaje, nizigaweje, niandike nini na mengine ya aina hiyo.

Lakini lengo halikuwa hilo, bali lengo limekuwa kuandika kila siku, kwa kushirikisha kitu muhimu kwenye safari yetu ya mafanikio. Na kilichobaki hapo ni historia. Sikai chini kujiumiza 800 au 1000 nitaifikia lini, badala yake nakaa chini na kutafakari kipi muhimu ambacho nasukumwa kumshirikisha rafiki yangu leo.

Na leo nilipoandika kwenye kichwa cha habari hapo UKURASA WA 801, ikanijia kwenye mawazo kwamba kipo kitu naweza kumshirikisha rafiki yangu kuhusu hizi kurasa zaidi ya 800. Yapo mengi sana lakini naomba nikushirikishe yale machache muhimu.

  1. Usiangalie mwisho, bali angalia njia.

Watu wengi wanapoweka malengo, huangalia mwisho kama ndiyo kila kitu. Hii inawafanya wahamishe furaha yao, kwamba hawawezi kuwa na furaha sasa mpaka watakapofikia lengo lao.

Sasa mimi kwenye hizi makala sina lengo la mwisho, ni kuandika kila siku, na ninaposhirikisha ujumbe wangu wa siku, nimekamilisha zoezi la siku, tutaendelea tena kesho.

  1. Hakuna mlima mgumu kupanga, kama upo tayari kupiga hatua moja.

Hata mlima uwe mkali kiasi gani, unaweza kupandika kama utakuwa tayari kupiga hatua moja. Watu wengi wanaangalia mlima ulivyo mkali na kuchoka kabisa, wanashindwa hata kuanza. Lakini ukianza kwa hatua moja, lazima ufike mbali.

Mlima hapa namaanisha chochote kikubwa unachotaka kufanya, iwe ni biashara, kazi, uandishi, sanaa na mengine. Kuwa tayari kupiga hatua moja, halafu nyingine na nyingine. Unachohitaji ili safari ikolee, ni kuweka mguu mmoja mbele ya mwingine, na kurudia zoezi hilo mara nyingi.

  1. Kitu ambacho ni muhimu kwako, kifanye kila siku.

Kama kuna kitu muhimu sana kwako, kama kipo kitu ambacho unataka kuwa bora zaidi, basi kifanye kila siku, ndiyo, yaani kila siku. Siyo ufanye siku unayojisikia, siyo ufanye siku ambayo una hamasa, badala yake fanya kila siku.

Unapofanya kitu kila siku, inajijenga na kuwa tabia, na hivyo kuwa rahisi zaidi kwako kuendelea kufanya.

Kurasa 800 ukiziangalia kwa mbali ni nyingi, lakini ukianza kuandika kila siku, hakuna wingi wa kukutisha, ni sehemu ya maisha. Kadhalika kwenye kujenga biashara kubwa au chochote. Ukiangalia kwa nje utasema hii kubwa sana, haiwezekani, lakini ukianza kufanya, utaona unafika unakotaka kufika.

Anza kupiga hatua rafiki yangu, na chochote kisikurudishe nyuma.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.