UKURASA WA 802; Kama Ndiyo Ungekuwa Unaanza Leo…

By | March 12, 2017

Business as usual ni usemi ambao umekuwa unatumika na wazungu kuashiria kwamba mambo yanafanyika kama kawa. Yaani leo watu wanafanya kwa sababu ndivyo walivyofanya jana, na juzi pia. Kwa kifupi ndivyo walivyozoea kufanya, ndivyo ilivyozoeleka kufanya.

IMG-20170301-WA0001

Hali hii imekuwa inapelekea kazi nyingi kudumaa, biashara nyingi kufa na hata watu kuyachoka maisha yao. Hii ni kwa sababu hakuna kipya kinachowavutia, na pia mabadiliko yanapotokea yanawafanya watu hawa kubaki nyuma, kwa sababu hawakuyaona mabadiliko hayo haraka.

Kuna hotuba moja imewahi kuwatoa watu machozi, ilikuwa hotuba iliyotolewa na aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya simu ya nokia, wakati kampuni hiyo inachukuliwa na kampuni ya microsoft baada ya kushindwa kujiendesha.

Najua kama umeanza kutumia simu mwanzoni mwa miaka ya 2000, utakuwa ulianza kwa kutumia simu ya nokia, na huenda mpaka sasa unatumia nokia. Mimi nina simu ya nokia ndogo ambayo nimeitumia kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, imekuwa inaanguka, naiokota na maisha yanaendelea. Ilikuwa kampuni kubwa na imara, lakini ikaishia kushindwa kujiendesha.

Katika hotuba hiyo ya kutoa machozi, mkurugenzi alisema; hatujafanya kosa lolote, lakini tumeishia kupoteza. Na ukiangalia ni kweli, kwa business as usual, hawakuwa wamefanya kosa lolote, kwa sababu walikuwa wanafanya kama walivyozoea kufanya. Walichofanya jana ndiyo walichoendeleza kesho yake. Na hili ndiyo kosa kubwa ambalo hawakuliona, na huenda wewe pia hulioni kwenye kazi au biashara yako.

Kuna kitu kinaitwa mabadiliko, hiki ni kitu ambacho kinatokea kila siku na kinamhusisha kila mtu. Hivyo usipobadilika haraka, unaachwa nyuma, hata kama hujafanya kosa lolote. Hivyo kufanya mambo kwa mazoea, ni kujiandaa kushindwa na kupoteza.

SOMA; Nenda Kinyume Na Sababu Ulizonazo, Leo Tu…

Hivyo rafiki yangu, katika kuhakikisha huishii kupoteza kama walivyofanya nokia, kushindwa kuchangamkia teknolojia mpya za simu zilizokuja, nimekuandalia swali muhimu la kujiuliza kila siku.

Swali hilo ni; kama ndiyo ningekuwa naanza kufanya leo, je ningeendelea kufanya? Kila unapoianza siku yako, angalia yale uliyofanya jana na siku zilizopita, na kabla ya kuendelea kufanya kama ulivyozoea, jiulize je kama ndiyo ungekuwa unaanza kufanya leo, ungeanza? Au mazingira yameshabadilika sana? Kwa kuangalia hivyo utaona mambo mengi ya kubadili, na yafanyie kazi kila siku.

Usiwe mtu wa kufanya kazi, biashara na hata kuendesha maisha yako kwa mazoea. Kila siku chukulia kama ndiyo unaanza, na usiogope kufanya maamuzi hata kama ni ya kuanza upya. Mabadiliko hayana huruma, hayaangalii wewe umekuwa mtiifu kwa kazi au biashara yako kiasi gani, kama hujabadilika unaachwa nyuma.

Badilika leo rafiki, kabla hujachelewa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.