UKURASA WA 814; Wamekijua Leo, Walikitaka Jana…

By | March 24, 2017

Mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani, hasa enzi hizi za ukuaji wa sayansi na teknolojia, yanagusa kila kona ya maisha yetu. Sehemu inayoguswa zaidi na ambayo wengi hawaioni vizuri ni kwenye biashara.

IMG-20170319-WA0002

Njia za ufanyaji wa biashara zimebadilika sana. Kuanzia kutangaza biashara, kuwafikia wateja na hata mahitaji yenyewe ya wateja. Kabla ya ukuaji huu wa kasi wa teknolojia, biashara ziliongozwa na mahitaji. Unaangalia watu wanataka nini na kuwapatia.

Lakini ukuaji huu wa teknolojia, unatoa fursa ya kuwapa watu kitu ambacho hata bado walikuwa hawajui kama wanakitaka. Yaani unakuja na bidhaa au huduma ambayo watu walikuwa hawajui kama wanaitaka, lakini wanapoanza kuitumia wanaona thamani yake na kuitaka zaidi.

Hivi ndivyo inavyotokea na ilianzia kwenye mitandao ya kijamii. Watu wengi sana sasa hivi wanatumia mitandao ya kijamii kama facebook na wasap. Lakini miaka 20 iliyopita mitandao hii haikuwepo kabisa, na hakuna mtu amewahi kulalamika kwamba hakuna mitandao, kwa kipindi hicho. Maisha yalikuwa yanakwenda kama kawaida.

SOMA; Kujua Na Kufanya…

Lakini sasa watu wamejua uwepo wa mitandao hii, wakiikosa kwa dakika chache tu hapakaliki. Yaani ikatokea mtandao siyo mzuri na wakashindwa kufikia mitandao hii, wanaona kama kuna kikubwa wanakikosa.

Hii ndiyo dhana ya wamekijua leo, walikitaka jana. Yaani watu wamejua kitu leo kwamba kipo na wanaweza kukitumia, ila wanagundua kwamba walikitaka kitu hicho jana, yaani ni kama wameshachelewa na hivyo wanakitaka kwa ubora wa hali ya juu sana.

Dhana hii unaweza kuitumia kwenye biashara yako, kwa kuangalia thamani gani unaweza kuongeza kwenye biashara yako ambayo huenda wateja wako kwa sasa hawaoni, ila wakishajua watapenda zaidi. Inawezekana wateja hawakuulizi chochote kwa sasa, kuhusu huduma hiyo mpya unayoweza kutoa, lakini utakapoanza kutoa utashangaa unapokea malalamiko unapochelewa kufanya.

Kwa zama tunazoishi, kila biashara ina nafasi ya kuwashangaza wateja wako, fanya hivyo pia kupitia biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea MTAALAMU NETWORK

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.