UKURASA WA 857; Hakuna Anayejali Zaidi Yako….

By | May 6, 2017

Kuna makosa makubwa sana huwa tunayafanya kwenye kujali, tunafikiri wapo watu wanajali sana kuhusu sisi na maisha yetu kuliko hata tunavyojijali sisi wenyewe. Hili ni kosa tunalorudia mara kwa mara na linazalisha matatizo makubwa kwetu, au kutuzuia kupata kile ambacho tunakitaka.

IMG-20170218-WA0000

Kwanza tunashindwa kufanya yale ambayo tunataka kufanya, kwa kuona wengine watatushangaa, wataona labda tunakosea, au kama ikitokea tukashindwa basi watatudharau. Huenda mtu ametupa maoni mabaya juu ya kile tunachofanya, na hivyo kuamua kuacha kufanya, kwa kufikiri anajali sana juu ya kile tunachofanya. Tunachosahau ni kwamba, mtu huyu hakosi usingizi kwa sababu sisi tunafanya kitu fulani au tumeshindwa kitu fulani. Tunasahau kwamba kwa sisi kufanya kitu, au kushindwa kitu, hakuwafanyi watu wasahau matatizo yao na kuanza kujali kuhusu sisi. Watu bado wana shinda na matatizo yao, na hivyo ndiyo vitakuwa vipaumbele vyao, siyo sisi.

Pili tunafikiri kwa sababu watu wana mamlaka fulani, au wajibu au kwa sababu tumewaambia wafanye kitu, basi wanajali sana kuhusu sisi. Hapa ndipo tunalaumu serikali au taasisi fulani ambazo zilipaswa kufanya kitu fulani lakini hazikufanya. Au umemwajiri mtu afanye kitu fulani na hakufanya, au hakufanya kwa viwango ulivyotaka wewe. Tunalaumu kwa sababu tunafikiri watu hawa wanajali mno, kwamba wanasahau kila kitu chao na kupeleka mawazo yao yote kwenye kile tunachotaka sisi.

SOMA; Kujali Kunakoumiza…

Ukweli ni kwamba, kama sisi wenyewe, hatutaweka vipaumbele vikubwa kwenye maisha yetu na kwenye kile ambacho tunataka, tutaishia kulaumu wengine kwa makosa ambayo siyo yao. Watu wanawaza yao zaidi ya wanavyowaza yetu. Kwa asili sisi binadamu ni wabinafsi, hivyo kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yetu ni kuhakikisha sisi wenyewe tuko vizuri kwanza.

Hivyo rafiki yangu, chochote unachotaka, pambana ili uweze kukipata. Usidhani tu kwa sababu kuna mtu anafanya basi atafanya kweli, au atafanya unavyotaka. Usidhani anayekukatisha tamaa ataenda kukosa usingizi kwa sababu ya mambo yako. Hakuna. Kila mtu anajali yake zaidi, jali yako zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.