UKURASA WA 856; kisichofanywa na wengi….

By | May 5, 2017

… kwa sababu labda ni kigumu, au bado hawajakiona, au siyo maarufu sana, lakini kina thamani kwa wengine, kinatatua shida za wengine au kina uhitaji kwa watu, ndiyo kinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako kufanya.

IMG-20170314-WA0003

Hichi pia ni kipimo kizuri kwako, kujua kama upo kwenye njia sahihi ya kufanikiwa au la. Kwa sababu ukishajikuta upande wa wengi, jua kabisa kwamba mafanikio kwako hayapo, au yatachukua muda sana. Kazana sana kuwa upande wa wachache, na siyo kwa sababu wengi ni wabaya, ila kwa sababu wengi hawapendi shida, wengi hawapendi vitu vigumu, hivyo kukimbilia vitu rahisi, ambavyo kila mtu anafanya.

Kitu kikishakuwa kinafanya na kila mtu, mara moja thamani yake inashuka. Kikishakuwa rahisi kupatikana hakuna anayehangaika nacho, kwa sababu kipo, hakuna mwenye haraka nacho. Ila kikiwa kigumu, kikawa adimu, kikawa kinapatikana eneo fulani tu, hapo thamani yake inakuwa kubwa, watu hawasubiri, wanakitaka na wanakitaka sasa.

Unaonaje hali hiyo ikawa kwako wewe, kwa kufanya kitu ambacho watu hawawezi kukipata kwingine bali kwako tu. Na hivyo kutokuwa na subira pale wanapoipata nafasi ya kukipata. Sasa rafiki, hali hii haiji kama ajali, bali itatengenezwa.

SOMA; Tabia Moja Inayowaingiza Watu Wengi Kwenye Madeni Ya Kifedha, Na Namna Ya Kuiepuka.

Wapo wanaosema kwa dunia ya sasa kila kitu kimeshafanywa hivyo hakuna namna unaweza kuwa wa tofauti na wa kipekee kabisa, na mimi nawaambia siyo kweli. Hicho hicho ambacho unaona kinafanywa na kila mtu, unaweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana na ukatengeneza thamani ambayo haikuwepo hapo awali. Wewe pekee ndiyo ukawa unatoa thamani hii na watu wakaipenda sana kutoka kwako.

Unasubiri nini rafiki kujitofautisha, anza kwa kuangalia kile ambacho watu wanakosa, na hakuna aliye tayari kufanya. Kuwa tayari wewe na tengeneza soko lako jipya, ambalo utalihodhi wewe mwenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.