UKURASA WA 869; Kama Haiumizi, Haina Thamani…

By | May 18, 2017

Swali; ni mchezo gani ambao unapenda kuufuatilia sana? Mchezo ambao ukiwa unachezwa basi lazima utafuatilia hata kujua matokeo tu, kama huna muda wa kuangalia mchezo wote?

Kwa watu wengi, upo mchezo ambao wanapenda kuufuatilia, inawezekana ni mpira wa miguu, ambao wengi wanafuatilia, mchezo wa ngumi, riadha, mpira wa kikapu, mieleka na kadhalika.

Sasa swali la pili linakuja, umewahi kuangalia kwa makini wachezaji wa mchezo unaopenda wanapokuwa uwanjani? Namna wanavyoanguka, wakikazana kushinda ili wao na wewe mfurahie? Je umewahi kupata nafasi ya kuwaangalia wakiwa wanafanya mazoezi? Namna ambavyo wanakazana ili wawe bora uwanjani na waweze kushinda?

Kama umeweza kuona hayo niliyokuuliza hapo juu, basi kuna kitu kimoja utakuwa umekiona, kitu hicho ni maumivu. Wachezaji wote wanaumia sana ili waweze kuwa bora, wanafanya mazoezi makali ili kuboresha mbinu zao za michezo. Wanaumia misuli kwa kuchoka na mazoezi. Na hata wanapokuwa uwanjani wanaanguka na hata kuumizwa na wenzao katika kupambana ili kushinda. Na wewe unafurahia ushindi unaopatikana, bila ya kujali kwamba wenzako wameumia.

Tunaweza kusema kwamba, furaha yako wewe ni maumivu ya wengine. Kadiri wachezaji wale wanavyokazana ili kushinda, ndivyo wanavyoumia. Lakini wao hawawazi sana maumivu yale, bali wanachowaza ni kile wanachotaka wao. Hivyo kwa kujua kile wanachotaka, maumivu yanakosa nafasi na wanapambana.

SOMA; Usipunguze Bei, Ongeza Thamani…

Nimekuambia hili leo kukukumbusha vitu viwili;

Kwanza kufanya kitu chochote cha thamani, kitu chochote kikubwa, ambacho kinaongeza thamani kwako na kwa wengine, maumivu hayaepukiki. Hakuna namna unaweza kuwa mkuu bila ya kuumia, na kadiri unavyotaka kufika mbali, ndivyo utakavyoumia zaidi. Hivyo usiogope kuumia kama unataka ukuu.

Pili; ukijua kile unachotaka, na namna ya kukifikia na kikawa na maana kubwa kwako na kwa wengine, maumivu hayataweza kukuzuia. Licha ya maumivu utaendelea kupambana kwa sababu unaona dhahiri ni wapi unapotaka kufika na unajua utafikaje pale. Mengine yote yanakosa maana na unakuwa tayari kupambana. Hivyo jua wapi unataka kufika na jua maana ya kufika pale kwako binafsi na kwa wengine pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.