UKURASA WA 878; Wape Watu Suluhisho…

By | May 27, 2017

Bill Cosby amewahi kunukuliwa akisema; hajui ufunguo wa mafanikio, ila anajua ufunguo wa kushindwa ambao ni kujaribu kumridhisha kila mtu.

Watu wengi wamekuwa wanapenda kuwaridhisha wengine, ili waonekane wema, wakijua kufanya hivyo ndiyo watakubalika zaidi na kuweza kufanikiwa kwenye lolote wanalotaka. Huo siyo ukweli hata kidogo. Kujaribu kumridhisha kila mtu, ni njia ya uhakika ya kushindwa. Kutaka kila mtu akubaliane na wewe, inabidi usifanye chochote kikubwa, na hapo wapo pia ambao hawatakubaliana na wewe.

Ili kufanikiwa, lazima ufanye mambo makubwa, lazima ufanye mambo ambayo hayajazoeleka, lazima ufanye kile ambacho wengine hawawezi au hawapo tayari kufanya, na hilo litawafanya wasijisikie vizuri, hivyo watakupinga na kukukatisha tamaa.

Ninachotaka kukuambia leo ni kwamba badala ya kufikiria utawaridhishaje watu, angalia ni kitu gani kikubwa unaweza kufanya. Toa suluhisho kwa matatizo ambayo watu wanayo. Toa suluhisho kwa watu wengi, boresha maisha ya watu wengi ambao wana shida unayoweza kuitatua. Na achana na wale wachache ambao watakuwa wanakupinga na kukukatisha tamaa. Hata hivyo hawana kubwa la kufanya ndiyo maana wanatumia muda wao kukupinga wewe.

SOMA; Tatizo Na Suluhisho…

Fanya kitu kikubwa kwa ajili ya wengine, siyo wote watafurahia, ila wanaonufaika watafurahia na watakuwa pamoja na wewe. Kupitia kazi unayofanya, biashara unayofanya na maisha unayoishi, jiulize ni thamani gani zaidi unatoa kwa wengine, jiulize unayafanyaje maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Na hapo ndipo unapoweza kuziona fursa za kufanya zaidi. Lakini hii ni kama utaacha kujaribu kumridhisha kila mtu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.