UKURASA WA 890; Unachoona Ni Sahihi?

By | June 8, 2017

Huwa tunaamini sana kile tunachoona, lakini je tunachoona ni sahihi?

Hili ni swali muhimu sana kujiuliza kila wakati. Kabla hujajipa uhakika wa kile ambacho unakiona, jiulize kwanza kama unachoona ni sahihi.

Unaweza kushangaa kwa nini nakuuliza hivyo wakati unaona mwenyewe? Je inawezekana ukajidanganya mwenyewe kwa unachoona?

Jibu ni ndiyo, unajidanganya kila wakati kwenye kile unachoona.

Kwani mara nyingi huwa hatuoni kitu kama kilivyo, bali tunaona kile ambacho tunataka kuona. Sijui umenielewa vizuri hapo?

Unachoona, japo ni kwa macho yako au ufahamu wako, lakini kinaathiriwa na kile ambacho unajua au kutaka wewe.

Unajua usemi maarufu kwamba macho hayawezi kuona kile ambacho ubongo haujui? Usemi huu ni kweli na ndiyo unaofanya kile tunachoona kisiwe halisi.

SOMA; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…

Taarifa tunazokuwa nazo awali, kabla ya kuona kitu, au imani tulizonazo juu ya kitu, zinaathiri sana kile ambacho tunaona.

Kwa mfano, mtu akipata ugonjwa wa akili, kama inavyojulikana kama kichaa, kwa jamii zinazoamini kwenye imani za kishirikina watasema amelogwa. Lakini kwa jamii zinazoamini kwenye sayansi watasema anaugua ugonjwa wa akili. Mtu ni yule yule matendo yale yale lakini watu wanaona vitu tofauti.

Ni muhimu kujikumbusha hili, kwa sababu namna unavyoyaona mambo, inaweza kuwa kikwazo kwa mafanikio yako. Kwa mfano kama unafikiria biashara ni ngumu na haifai, utajikuta unaona kila aliye kwenye biashara anapata matatizo na kupata hasara. Kwa sababu hicho ndiyo unataka kuona wewe, ili imani yako iwe sahihi. Lakini kama unaamini biashara ni nzuri na zina mafanikio, utaona wafanyabiashara wengi wenye mafanikio. Utaona kinachokamilisha imani yako.

Na hivyo ndiyo ilivyo kwenye karibu kila kitu kwenye maisha yetu, tunachoona kinakamilisha imani yetu. Hivyo kama tunataka kuuona ukweli kama ulivyo, tuangalie kwanza tunaamini nini kwenye kile ambacho tunaangalia. Hapo utaona kama utaweza kukubaliana na kile ambacho unaona. Lakini sasa, unahitaji kuwa makini ili kuweza kuona hilo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.