UKURASA WA 891; Fedha Ni Fedha…

By | June 9, 2017

Wapo wanaosema fedha ni mbaya,

Na wapo pia wanaosema fedha ni nzuri.

Na wote hao wanakosea kabisa, kwa sababu fedha ni fedha.

Fedha siyo mbaya, wala fedha siyo nzuri, fedha ni fedha.

Fedha inaweza kutumiwa kufanya mabaya, vile vile fedha inaweza kutumiwa kufanya mazuri, lakini bado inabaki kuwa fedha.

Hivyo unapoiangalia fedha, usiihusishe na chochote unachoona, maana fedha yenyewe haina nguvu bali inapewa nguvu ya kufanya na yule aliyeishika fedha hiyo.

Najua hili ni gumu kueleweka, hasa unapolisikia kwa mtu ambaye anakuambia kila siku ni muhimu ufanye kazi kupata fedha na kuwekeza ili kufikia uhuru wa kifedha. Na tatizo ni kwamba linapokuja swala la fedha, tunaweka hisia mbele kuliko fikra.

SOMA; Tabia Moja Itakayokuwezesha Kudhibiti Matumizi Ya Fedha Zako.

Mara nyingi tunapoona kile ambacho watu wamefanya na fedha zao, tunaweka hisia mbele na kuihusisha fedha na kile ambacho kimefanyika. Unapokuta mtu tajiri akiwanyanyasa watu, utasema pesa imemharibu, lakini wapo watu wengi ambao hawana fedha na wanawanyanyasa watu.

Hivyo rafiki, tuitafute fedha, na tuitumie kufanya mambo mazuri. Na ndiyo maana ninakusisitiza kila siku kuwa bora wewe mwenyewe kwanza. Kama kuna tabia unazo ambazo siyo nzuri, zifanyie kazi, kwa sababu fedha inachofanya ni kuchochea kile kilichopo ndani yako, na siyo kuleta kimya.

Na unapomwona mtu kafanya mazuri au mabaya, jikumbushe ya kwamba siyo fedha inafanya vile, bali ni mtu anafanya. Fedha imetumika tu.

Fedha ni fedha, mazuri na mabaya yanafanywa na watu, kwa kutumia fedha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.