UKURASA WA 903; Njia Bora Ya Kuwapima Wanaokuzunguka Kama Wanakufaa…

By | June 21, 2017

Maisha yako ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka, huu ni ukweli ambao watu wengi huwa hawapendi kukubaliana nao. Kwa sababu huwa tunapenda kuona tuna uwezo mkubwa kuliko uhalisia. Kama ambavyo ulipokuwa mtoto wazazi walikukataza kucheza na watoto fulani kwa sababu ya tabia zao mbaya, nina hakika uliwaambia au ulijiambia, mimi nacheza nao tu, siwezi kuchukua tabia zao.

Lakini nguvu ya wale wanaotuzunguka ni kubwa sana kwetu. Mambo mengi tunayofanya au tunayoacha kufanya, wale wanaotuzunguka wanahusika kwa sehemu kubwa.

Ukizungukwa na watu wa kawaida, watu wanaofanya mambo kwa mazoea, wasio na ndoto kubwa kwenye maisha yao, na wewe utaishia kuwa na maisha ya aina hiyo. Lakini ukizungukwa na watu wenye ndoto kubwa, wanaoweka juhudi kubwa ili kuweza kufanya makubwa, na wewe utalazimika kuwa na ndoto kubwa na kuweka juhudi kubwa. Ni asili ya binadamu.

Sasa huenda umekuwa unasikia hili lakini hujui ulifanyieje kazi. Au huenda hujajua vizuri wale wanaokuzunguka wana ndoto gani kubwa kwenye maisha yao. Hivyo itasaidia kama utaweza kuwapima. Kwa sababu kuna uwezekano usiwe karibu na watu ambao tayari wameshafanya makubwa, lakini kuwa na wale wanaoenda kwenye makubwa, itakusaidia zaidi.

SOMA; Njia Tano (05) Bora Za Kutoa Mafunzo Kwa Wafanyakazi Wa Biashara Yako.

Watu ambao tayari wameshafanya makubwa, au ambao wanaamini kwenye kufanya makubwa, ukiwaomba ushauri wa namna ya kufanya mambo makubwa, kamwe hawatakukatisha tamaa. Hata kama ni vigumu kiasi gani, watakuambia ukweli ulivyo, halafu watakupa moyo wa kufanya. Lakini watu ambao hawajawahi kufanya makubwa, na hawaamini kwenye makubwa, waombe ushauri kwenye jambo lolote kubwa na kikubwa watakachofanya ni kukukatisha tamaa.

Kujua wale wanaokuzunguka kama wameshafanya makubwa au wanaamini kwenye kufanya makubwa, waombe ushauri wowote kuhusu kufanya jambo kubwa kabisa. Jambo ambalo hata wewe mwenyewe linakupa wasiwasi, lakini waombe ushauri, na uone wanapokeaje kile umewauliza. Kama watakimbilia kukukatisha tamaa, jua hao siyo watu wazuri kukuzunguka, hata kama sababu zao zitakuwa nzuri kiasi gani.

Kama mtu hajawahi kufanya jambo lolote kubwa, na haamini kwenye uwezo wa kufanya makubwa, atahakikisha wale wanaomzunguka na wao wanakuwa kama yeye. Sasa pata picha umejikuta katikati ya watu watano wa aina hiyo, huwezi kupiga hatua kwenye jambo lolote kubwa.

Kuwa makini sana na wale wanaokuzunguka, ndiyo wamekufikisha hapo ulipo sasa. Hivyo kwenda zaidi ya hapo ulipo, angalia waliofika au wanaokwenda mbali zaidi ya hapo ulipo. Halafu ongozana nao.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

One thought on “UKURASA WA 903; Njia Bora Ya Kuwapima Wanaokuzunguka Kama Wanakufaa…

  1. Pingback: UKURASA WA 1023; Tatizo Siyo Waliokuzunguka, Tatizo Ni Wewe… – Kisima Cha Maarifa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.