UKURASA WA 911; Maamuzi Ya Mtu Mmoja….

By | June 29, 2017

Kama maamuzi ya mtu mmoja yanaweza kuharibu na kuvuruga kabisa maisha yako, nina habari mbaya kwako, huna maisha.

Huo ndiyo ukweli, japo unaweza usiupende, kwa sababu ukweli huwa unaumizwa.

Unapaswa kutengeneza maisha ambayo yanaweza kujiendesha vizuri, changamoto zipo na vikwazo vipo, lakini maamuzi ya mtu mmoja yanapokuwa na athari kubwa kwako, upo kwenye wakati mgumu zaidi.

Maamuzi ya mtu mmoja kuathiri maisha yako ni kama pale unapokuwa umeajiriwa, na chanzo chako pekee cha kipato ni mshahara, halafu pia una madeni ambayo unategemea mshahara huo kuyalipa. Hapo mwajiri akifanya maamuzi ya kukufukuza au kukusimamisha kazi, maisha yako yanavurugika kwa kiasi kikubwa.

Hata kwenye biashara pia, unaweza kuwa kwenye wakati mgumu iwapo una mteja mmoja mkubwa, au anayekusambazia ni mtu mmoja pekee. Hii inakuweka wewe kwenye wakati mgumu pale anapositisha huduma yake, iwe ni kununua au kukusambazia bidhaa.

SOMA;  Maamuzi Yoyote Ni Bora…

Huwezi kuwa na maisha yenye uhuru iwapo utakuwa unahofia maamuzi ya mtu mmoja, ambayo yanaweza kuathiri maisha yako.

Leo fanya tafakari ya kina kwenye maisha yako, na uone ni maeneo gani ya maisha yako ambayo umetoa nguvu kubwa kwa mtu mmoja au watu wachache. Kisha chukua hatua ya kununua uhuru wako.

Na namna ya kununua uhuru ni kutafuta njia zaidi ili usiwe na utegemezi wa mtu mmoja au eneo moja. Kama ni kipato basi hakikisha una njia nyingi za kuingiza kipato na siyo moja pekee.

Ondoa kabisa utegemezi mkubwa wa eneo la maisha yako kwa mtu mmoja au wachache. Kila mara hakikisha una maeneo mengi unayotegemea kupata kitu, hali hiyo pekee inakupa kujiamini na hata nguvu ya kujadiliana pale maslahi yako yanapokuwa kwenye wakati mgumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.