UKURASA WA 913; Vikwazo Vya Wengine, Ni Fursa Nzuri Kwako…

By | July 1, 2017

Watu wanasema, moja ya kazi kubwa ambayo kila mtu anayo hapa duniani, ni kuweza kuishi na wengine. Changamoto nyingi tunazokutana nazo kwenye maisha, zinahusisha watu wengine. Kuna wakati unaweza kuona kabisa kama wengine ndiyo wamekuweka hapo ulipo sasa, wanakuzuia usipige hatua.

Labda ni mwajiriwa mwenzako ambaye amekuwa kikwazo kwako kwenye kila unachofanya, au hata bosi wako, na wakati mwingine mwajiri wako.

Labda ni mfanyabiashara mwingine, anayefanya biashara kama yako, ambaye anakuletea wakati mgumu. Anakuharibia biashara yako ili kukuza yake.

Labda ni mwenza wako, mtu ambaye mlipendana kweli, mkakubaliana kuishi pamoja, lakini baada ya hapo maisha yamekuwa ni changamoto kwako kila siku.

SOMA; Tafuta Vikwazo Unavyoweza Kuvivuka…

Japo unaweza kuona vikwazo hivi vinakurudisha nyuma, kwa upande mwingine ni fursa nzuri kwako.

Iko hivi rafiki, watu huwa hawakui mpaka wakutane na ugumu au changamoto. Ukitumbukizwa kwenye maji marefu leo hii, hata kama hujawahi kuogelea, hutasubiri tu kuzama, badala yake utaanza kutafuta namna ya kutoka pale.

Hivyo vikwazo na changamoto zote unazopitia kwenye maisha ni fursa ya wewe kukua, ni fursa ya wewe kujifunza kwamba mambo siyo rahisi, ni fursa ya kujenga uvumilivu na muhimu zaidi ni fursa ya kujifunza kuchukua maamuzi magumu, ambayo wengine hawawezi kuyaelewa.

Unapokuwa na watu ambao wanakuwekea vikwazo na kukusababishia matatizo, usiishie tu kulalamika na kuona kama huna la kufanya. Badala yake tumia fursa hiyo kuwa bora zaidi, tumia fursa hiyo kuchukua hatua kubwa zaidi. Na pia chukua fursa hiyo kujifunza ili usirudi kwenye hali kama hiyo siku zijazo.

Wakati mwingine watu wanapokunyanyasa na kukutesa ndiyo wanakupa hasira ya kutoka chini yao na kwenda kufanya mambo yako, kwenda kujitegemea wewe mwenyewe. Zipo fursa nyingi kwenye kila hali unayopitia, unachohitaji ni wewe kuchukua hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.