UKURASA WA 914; Wakati Sahihi Wa Kuondoka….

By | July 2, 2017

Kwenye kila jambo tunalofanya kwenye maisha yetu, kuna wakati tunapaswa kuondoka. Kuondoka ama moja kwa moja na kwenda kufanya mambo mengine, au kuondoka kwa kubadilika na kufanya kwa njia mpya na viwango vipya.

Lakini wengi wamekuwa hawajui upi wakati sahihi wa kuondoka, na hivyo kujikuta kwenye changamoto ambazo zinawarudisha nyuma, au kuwazuia kufanikiwa.

Ni kawaida ya binadamu kupenda mazoea, wote tunapenda kufanya kile ambacho tumezoea kufanya. Kujaribu mambo mapya ni hatari, kwa sababu iwapo yatashindwa, tutakuwa tumejiangusha wenyewe. Ni fikra zinazoonekana nzuri, mpaka pale unapokuwa umechelewa kiasi kwamba kutokuondoka au kubadilika kwako, kunakugharimu.

Matatizo ya muda wa kuondoka au kubadilika yapo mawili;

Tatizo la kwanza ni kuondoka mapema, kuondoka kabla ya muda. Hapa unaondoka na kuacha fursa zikiwa bado mbichi kabisa na hivyo kutopata marejesho sahihi kulingana na juhudi ulizoweka. Kwa mfano umeanzisha biashara, ikaenda kiasi kwa changamoto, baadaye ukaona haizalishi na kuifunga. Halafu ukaacha kufanya biashara kabisa. Hapo unapoteza mafunzo mengi sana ambayo ulishayapata kuhusu biashara na hivyo hunufaiki kabisa. Lakini iwapo ungeendelea, au ungefanya biashara nyingine, usingekuwa sawa na mtu anayeanzia chini kabisa.

SOMA; Huhitaji Kila Mtu, Unahitaji Watu Sahihi…

Tatizo la pili ni kuchelewa kuondoka, yaani wakati unakuwa umekupita kiasi kwamba umeshapoteza sana na hata ukiondoka haina manufaa yoyote kwako. Kwa mfano ni biashara haikuendei vizuri, kila wakati ni changamoto. Kila wakati unapata hasara, mtaji unazidi kupungua, lakini upo tu, hakuna unachobadili. Unakuja kustuka mtaji umekata kabisa, huna tena namna ya kuendesha biashara hiyo, hivyo unafunga. Kama ungeshtuka mapema na kuchukua hatua, ungeweza kuokoa kifo cha biashara yako.

Kwa kuwa binadamu sisi siyo watabiri wazuri, ni vigumu kujua wakati gani sahihi wa kuondoka, na hivyo hatua muhimu ya kuchukua ni kuwa unajaribu mambo mapya kila wakati. Usiridhike na kujisahau na kitu kimoja unachofanya, hata kama kina manufaa makubwa kiasi gani. Pia endelea kuangalia kwa kina na kufuatilia kila kinachoendelea kwenye kila jambo unalojihusisha nalo. Kuanzia kazi, biashara, mahusiano, fedha, uwekezaji na maisha kwa ujumla.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.