UKURASA WA 918; Kuwa Hapa Sasa…

By | July 6, 2017

Wakati unasoma hapa sasa hivi, mawazo yako yanafikiria wapi? Yaani unakazana kukimbilia wapi, unamaliza kusoma hapa haraka ili uende wapi au ufanye nini?

Ni kawaida yetu binadamu kufanya mambo bila ya kuweka fikra na akili yetu yote kwenye jambo tunalofanya. Tunafanya kama tunapita, tukikimbilia kwenye jambo jingine.

Lakini ukikaa chini na kutafakari kwa kina, unaona huu wote ni ubatili na kupoteza nafasi muhimu tunazozipata kila siku. Tunapokuwa sehemu moja, lakini akili yetu inafikiria kitu kingine au sehemu nyingine, ni kupoteza hapa tulipo sasa. Tunakosa pale tulipo sasa, na hatuwezi kufaidi pale tunapopafikiria kwa wakati huo. Na hata tukienda kufanya lile tulilokuwa tunafikiria, akili yetu haitulii pale, tunakuwa na kingine tunachofikiria.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Mwaminifu Kwenye Ulimwengu Wa Sasa Uliojaa Kila Aina Ya Hila.

Kila wakati wa maisha yako ni wakati muhimu sana. Ni wakati unaostahili akili yako kuweka fikra zote pale. Ni wakati ambao unapaswa kuutumia vizuri kujifunza na hata kutoa mchango wako ambao utakufanya wewe na wengine kuwa bora zaidi.

Unapotenga hata dakika tano za kufanya kitu, hebu zitumie dakika hizo kufanya kitu hicho, huku akili yako, mwili wako na roho yako vikiwa pamoja kwenye kile unachofanya. Kuweka mwili kwenye kitu, huku akili na roho vikiwa sehemu nyingine, ni kujinyima haki ya kunufaika na pale tulipo.

Usikazane kung’ang’ana na kila kitu, badala yake weka kila ulichonacho kwenye kitu ulichochagua kufanya. Na kwa maana hii, lazima uwe na vipaumbele vikubwa kwenye yale unayopanga kufanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Category: KURASA ZA MAISHA

About Dr. Makirita Amani

Dr. Makirita Amani ni daktari wa binadamu, mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali. Dhumuni lake kubwa kwenye maisha ni KUWASAIDA WATU KUBORESHA MAISHA YAO NA KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA KUPITIA KAZI ANAZOFANYA. Mawasiliano 0717396253 email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.