Binadamu tuna tabia moja ya kushangaza sana, tukifanikiwa kufanya jambo zuri basi tunajiangalia sisi, tunaona namna gani tumejitahidi, jinsi gani tuna uwezo mkubwa, ni namna gani tuna bahati, na hata kujiambia na kuwaambia wengine kwamba tulijua tutaweza.
Lakini tunaposhindwa kufanya jambo, au tunapoanguka, tunawaangalia wengine, tunaanza kuangalia nani amehusika kwenye kushindwa kwetu, nani hakutupa ushirikiano tuliotaka, nani alikuwa kikwazo zaidi na nani hakupenda tufanikiwe.
Ni jambo la kushangaza sana, lakini ndivyo tulivyo, na hili limesababisha wengi kushindwa na kubaki chini.
Ili uwe mshindi, kwanza lazima ushindwe, halafu ukishashindwa sasa, ndiyo unajifunza somo muhimu sana kuhusu ushindi, kwamba hauji kirahisi, na hakuna atakayekupa kwa urahisi. Utajifunza kwamba ili kushinda hakuna yeyote unayemdai akupe au akuwezeshe kushinda, unapaswa kupokea kushindwa kama sehemu ya kujifunza na kutokurudia makosa uliyofanya awali.
SOMA; Anza Kuiua Biashara Yako Wewe Mwenyewe….
Sasa kama ukiwa ni mtu wa kutafuta nani kahusika na kushindwa kwako, kwanza utawaona wengi, na pili utabaki pale ulipo. Kwa sababu utapeleka mzigo kwa wengine na kujitoa wewe, ambaye ndiyo mhusika mkuu wa pale unapokuwa upo kwa wakati wowote wa maisha yako.
Kama ulishawahi kumwambia mtu… kama isingekuwa wewe ningekuwa mbali sana…. jua tu upo upande wa kupoteza. Kama bado una fikra za aina hiyo, achana nazo haraka, zitakuzuia wewe kupiga hatua.
Yamiliki maisha yako, miliki matendo yako, pokea matokeo yoyote unayoyapata, yamiliki, jifunze, chukua hatua kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog